Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI inaendesha kampeni maalum ya kusogeza huduma za afya za kibingwa katika hospitali za Halmashauri 184 Tanzania Bara.
Hayo yamesemwa na Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya Faraja Mgeni kwenye ufunguzi wa kambi ya matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi ya Dkt.Samia mkoani Ruvuma.
Madaktari bingwa 40 wameanza kutoa huduma za kibingwa katika Hospitali za Halmashauri zote nane mkoani Ruvuma,kuanzia Mei 6 hadi 10,2024
Mgeni amesema katika kipindi cha kuanzia Machi 2023 hadi kufikia Machi 2024 Wizara ya Afya kwa kushirikiana na TAMISEMI ilifanikiwa kuwajengea uwezo watoa huduma za afya Zaidi ya 4000 walioweza kutoa huduma za kibingwa kwa wananchi Zaidi ya 10,956.
“ ili kuimarisha huduma za afya kwa wananchi Wizara ya Afya na TAMISEMI inaendelea kuendesha kampeni maalum ya kusogeza huduma za afya za kibingwa katika hospitali za Halmashauri nchini,kampeni hii tunaianza leo Mei 6 na kukamilika Mei 28 mwaka huu na tutakuwa tumezifikia hospitali 184 zilizopo Tanzania bara’’,alisema.
Hata hivyo amesema katika Mkoa wa Ruvuma kampeni ya huduma za kibingwa inaanza Mei 6 na kukamilika Mei 10 mwaka huu na kwamba wananchi wanasogezewa huduma za kibingwa bobezi katika hospitali nane za Halmashauri mkoani Ruvuma.
Ametoa rai kwa Viongozi katika ngazi zote mkoani Ruvuma kushirikiana na madaktari bingwa hao na kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi ili kupata huduma hizo za kibingwa.
Kwa upande wake mgeni rasmi kwenye ufunguzi huo,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed ambaye aliwakilishwa na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Gilbert Simiya, ameipongeza serikali kwa kutoa madaktari bingwa na bingwa bobezi wa Dkt.Samia Suluhu Hassan ambao wamefika kutoa huduma za kibingwa mkoani Ruvuma.
Kanali Abbas ametoa rai kwa madaktari hao kufanya kazi yao kwa ufanisi mkubwa kwa kuwa serikali imeboresha upatikanaji wa vifaa tiba na kwamba serikali inaendelea kuboresha huduma za afya mkoani Ruvuma.
“Katika Mkoa wa Ruvuma serikali imetoa shilingi bilioni 18.721 kutekeleza miradi ya afya ikiwemo ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa,ujenzi wa hospitali za Halmashauri,vituo vya afya na zahanati’’,alisisitiza Kanali Abbas.
Ameitaja miradi mingine iliyotekelezwa mkoani Ruvuma ni ukarabati wa hospitali kongwe ya Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru,Mbinga Mji na ujenzi wa majengo ya huduma za dharura (EMD) katika hospitali za Tunduru,Nyasa,Madaba na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dr.Louis Chomboko akizungumza kwenye ufunguzi huo amesema madaktari bingwa hao wanatekeleza mpango kabambe wa huduma za mkoba nchini lengo likiwa ni kuboresha huduma za kibingwa karibu na wananchi katika ngazi ya Halmashauri.
Amewataja madaktari bingwa hao wanatoka katika hospitali za rufaa za mikoa,hospitali za Kanda,hospitali ya Taifa na maalum na kwamba huduma za kibingwa zinazotolewa ni ubingwa wa akinamama na uzazi,Watoto,upasuaji,magonjwa ya ndani,utoaji dawa za ganzi na usingizi.
Kampeni hii ya ina kauli mbiu ya madaktari bingwa wa Rais Samia tumekufikia karibu tukuhudumie ambayo imelenga kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma za kibingwa katika Halmashauri zao ili kuwapunguzia gharama za kusafiri umbali mrefu.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.