KAIMU Kamishina wa Ardhi Msaidizi wa Mkoa wa Ruvuma Ildeforce Ndemela amesema Idara ya ardhi mkoani Ruvuma imekusanya maduhuli ya serikali kwa asilimia 108.
Akitoa taarifa kwa Naibu Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt.Angelina Mabula,Kaimu Kamishina wa ardhi amesema kiasi hicho cha fedha kimekusanywa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020.
Ndelema amesema serikali iliupangia Mkoa wa Ruvuma kukusanya maduhuli ya serikali ya shilingi 990,000 hadi kufikia Juni 30,2020 na kwamba Idara ilifanikiwa kukusanya shilingi bilioni 1,076,957,355.22 sawa na asilimia 108.
“Katika mwaka wa fedha wa 2020/2021 Idara ya Ardhi Mkoa wa Ruvuma imepangiwa lengo la kukusanya kiasi cha bilioni 4.6, hadi kufikia Februari Mkoa umekusanya shilingi milioni 740 sawa na asilimia 16,mikakati ya kuongeza makusanyo ya kodi ikiwemo ikiwemo kuandaa na kusambaza ankra za umiliki na Hati za madai ya kodi’’,alisema Ndemela.
Hata hivyo amesema Mkoa wa Ruvuma katika kipindi mwaka 2020/2021 umepangiwa lengo la kupima viwanja 16,550 na mashamba 104 ambapo hadi kufikia Februari 22,2021,viwanja 4,873 na mashamba matano yamepimwa katika maeneo ya mijini na vijiji kwa ajili ya matumizi mbalimbali.
Amesema Idara hiyo imepokea jumla ya michoro ya mipango miji 41 yenye jumla ya viwanja 18,581 vya matumizi mbalimbali na kwamba zoezi la kurasimisha makazi holela linaendelea katika Halmashauri zote za Mkoa wa Ruvuma.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt.Angelina Mabula akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo amesema ukusanya maduhuri ya serikali kitaifa katika Wizara yake imefikia asilimia 30 na Mkoa wa Ruvuma umefikia asilimia 16.
Kutokana na hali hiyo Naibu Waziri Mabula ameziagiza Halmashauri zote nchini kuongeza juhudi za ukusanyaji maduhuli ya serikali ili kufikia malengo waliojiwekea ikiwemo kukusanya madeni kwa kuzingatia sheria.
“Sheria ipo wazi,kifungu cha 50 kifungu kidogo cha kwanza cha sheria ya ardhi namba nne kinampa siku 14 tu mdaiwa anapokuwa amepewa Ilani,ndani ya siku 14 asipoweza kulipa,tunampeleka kwenye Baraza, kinachofuata ni yeye kulipa deni’’,alisisitiza.
Amesema ikishatolewa oda ya kutakiwa kulipa anatakiwa kulipa au kukamata mali zake na kuuzwa ili fedha ipatikane ambapo amewataka watendaji wa Ardhi waache kugeuza ukusanyaji maduhuli kuwa kufanyika kisiasa.
Dkt.Mabula amewaagiza maafisa ardhi kuongeza kasi ya kupima viwanja na mashamba na kwamba hatua kali zitachukuliwa kwa maafisa ardhi watakaoshindwa kutekeleza majukumu yao ikiwemo upangaji, upimaji, umilikishaji.uthamini,usajili wa hati,utatuzi wa migogoro ya ardhi na ukusanyaji wa maduhuli ya serikali.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Machi,Mosi,2021
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.