JAJI Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma amesema,Serikali itaendelea kujenga na kuzifanyia ukarabati mahakama kongwe hapa nchini ikiwamo mahakama ya mwanzo Kigonsera wilaya Mbinga mkoani Ruvuma ambayo imeanza kuchakaa.
Profesa Ibrahim Juma alisema,lengo ni kuwa na mazingira mazuri ya kazi kwa watumishi na sehemu nzuri ya kupata haki kwa watanzania na mkakati wa kuboresha huduma zake.
Alisema hayo jana,wakati akizungumza na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya ya Mbinga wakiongozwa na mkuu wa wilaya hiyo Aziza Mangosongo baada ya kutembelea jengo la mahakama ya mwanzo Kigonsera wilayani humo akiwa katika ziara ya kujionea hali halisi ya mahakama na kuzungumza na watumishi.
Aidha alisema,ujenzi na ukarabati unaoendelea kufanyika katika mikoa mbalimbali nchini utakuwa kipimo kwa mahakimu na watendaji wengine wa mahakama kwa sababu watakuwa na mahali salama na bora katika utekelezaji wa kazi zao.
Profesa Juma alisema,mkakati huo ulioanza kutekelezwa miaka mitano iliyopita tayari umeonesha mafanikio makubwa kwa kuwa mahakimu wanafanya kazi kwa kuzingatia maadili,wananchi wanapata huduma bora na kupungua kwa malalamiko.
Jaji Mkuu, amevutiwa na hatua ya wananchi kutumia vyombo vya sheria kama vile mahakama kudai haki zao badala ya kujichukulia sheria mkononi, hivyo kuwezesha wananchi kutumia muda wao kufanya shughuli za maendeleo.
Amewataka wananchi na wadau wengine wa mahakama wilayani humo, kutoa ushirikiano kwa mahakama ili kufanikisha malengo waliyojiwekea ya kumaliza usikilizaji wa mashauri yanayofikishwa mahakamani kwa wakati.
Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, hayo yakitekelezwa serikali itapata muda mwingi wa kutekeleza miradi na shughuli mbalimbali za maendeleo, badala ya kujikita kushughulikia migogoro.
Mkuu wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Aziza Mangosongo alisema, maboresho yaliyofanywa na mahakama katika kipindi cha miaka mitano yamesaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza matukio ya uharifu katika wilaya hiyo kufuatia wananchi wengi kukimbia Mahakamani kutafuta na kudai haki zao.
Mangosongo ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya maadili ya Mahakama katika wilaya ya Mbinga, ameishukuru Mahakama kwa kuanza ujenzi wa mahakama ya mwanzo Matiri ambayo itakapokamilika itarahisisha usikilizaji mashauri kwa mahakimu.
Pia alisema,mahakama hiyo itasaidia sana kupunguza umbali mrefu wa wananchi kwenda maeneo mengine kusikiliza mashauri na kudai haki zao kupitia mhimili huo wa mahakama.
Mkuu wa wilaya alitaja changamoto kubwa katika wilaya hiyo ni masuala ya upelelezi wa kesi, lakini wanaendelea kuifanyia kazi ili kesi na mashauri yanayopelekwa mahakama yaweze kusikilizwa na kumalizika kwa wakati.
Mangosongo alisema, wananchi wengi wa Mbinga ni wakulima, kwa hiyo migogoro mingi inayotokea ni ya ardhi ambayo inafikishwa katika mabaraza ya kata na mara chache inafikishwa mahakamani.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mbinga mjini Jonas Mbunda,ameipongeza Mahakama nchini kufanya maboresho makubwa ya miundombinu, jambo lililohamasisha wananchi wengi kwenda mahakamani kutafuta haki zao.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.