Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma tarehe 14 Agosti, 2023 amezindua rasmi kikao cha kwanza cha Mahakama ya Rufani sambamba na ufunguzi wa Masjala ndogo ya Rufani katika Mahakama Kanda ya Songea hatua ambayo inatanua wigo wa upatikanaji wa haki karibu na wananchi.
Akizungumza wakati na Viongozi wa Mkoa wa Ruvuma kabla ya uzinduzi huo wa kihistoria Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Juma amesema kuwa, tukio hilo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama 2020/2021-2024/2025 katika kusogeza huduma ya utoaji haki karibu zaidi na wananchi, hivyo Mahakama imejipanga kukabiliana na changamoto ya umbali unaowalazimu wananchi kutumia gharama na muda mwingi kuifuata huduma ya haki.
“Siku ya leo ni siku ya historia kuanzia tulipoanza huduma ya Mahakama mwaka 1920 ambako Mahakama ya Rufani ilipatikana Dar es Salaam pekee. ambako Majaji walilazimika kutumia usafiri wa aina mbalimbali ili kupeleka huduma ya Mahakama ya Rufani kwa wananchi, lakini hivi leo huduma hii imefika hapa Songea,” ameeleza Jaji Mkuu.
Amesema kuwa, kuanzia sasa wananchi wa mkoa wa Ruvuma hawatalazimika kuifuata huduma ya Mahakama ya Rufani mkaoni Iringa bali huduma hiyo itapatikana ndani ya Kanda hiyo.
Msajili wa Mahakama ya Rufani (T), Mhe. Sylivester Kainda ameeleza kuwa jumla ya mashauri ya aina mbalimbali 34 yatasikilizwa katika kikao cha Mahakama ya Rufani ambacho kimezinduliwa leo na kusema kuwa uzinduzi huo ni nafuu kwa wananchi wa Mkoa huu ambao wengi walikuwa wakipiga simu kuomba mashauri yao yahairishwe kutokana na kutokuwa na nauli ya kufika Iringa ambapo yalikuwa yakisikilizwa kabla.
Amesema mashauri 34 yatasikilizwa kuanzia leo tarehe 14 Agosti, 2023 hadi tarehe 1 Septemba, 2023 na yatasikilizwa na Majaji wa Mahakama ya Rufani wakiongozwa na Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma ambaye ameambatana na Majaji wengine wa Mahakama ya Rufani ambao ni pamoja na Mhe. Dr Gerald Ndika, Mhe. Rehema Kerefu na Mhe. Sam Rumanyika.
Mhe. Kainda amesema kikao hicho cha Mahakama ya Rufani ,Masjala Ndogo ya Songea kitatumia wiki tatu kitasikiliza mashauri yanayohusu Rufani ubakaji Mauaji na matumizi madaraka ya madaraka.
Naibu Msajili Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Songea Elizabeth Nyembere amemshukuru Jaji Mkuu kwa uamuzi wake wa kuanzisha Masjala Ndogo ya Mahakama ya Rufani kwa kuwa itasaidia kupunguza gharama kwao na kwa wadau ambao walikuwa wakitumia fedha nyingi Kwenda Iringa.
Amesema watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Songea na wadau wataokoa fedha ambazo walikuwa wakizitumia kama nauli na posho kwa ajili ya kupeleka nyaraka na kufuatilia Rufani mkoani Iringa na hivyo fedha hizo kuelekezwa katika shughuli nyingine za utoaji haki.
“Hii ndio mara ya kwanza, kwa kweli tunapenda kumshukuru sana Jaji Mkuu kwa uamuzi wake ambao umewasaidia wananchi wa maeneo ya pembezoni kama vile Mbinga, Namtumbo kutoka kwao hadi Iringa kufuatilia Rufani zao…kwani kutoka hapo Songea hadi Iringa ni karibu ni Kilometa 400 bado hajatoka Mbinga na Namtumbo…hii ni Faraja kwetu na kwa wadau wetu kuwa na Masjala Ndogo hapo” amesisitiza.
Tukio hilo pia lilishuhudiwa na viongozi wa Mahakama ya Tanzania pamoja na Kanda ya Songea na Uongozi wa Mkoa wa Ruvuma ulioongozwa na Mkuu wa Mkoa, Kamati ya Ulinzi Mkoa na wageni mbalimbali.
Uzinduzi wa Masjala hiyo ndogo ya Mahakama ya Rufani inafanya zifike 17 baada ya ile iliyozinduliwa Mkoani Morogoro mwezi Aprili mwaka huu.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.