Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa watanzania hususani vijana kujiepusha na kutoa figo zao kwaajili ya kufanya biashara ili kuepuka madhara makubwa yanayoweza kujitokeza.
Makamu wa Rais amesema hayo leo tarehe 21 Julai 2023 akiwa ziarani mkoani Ruvuma mara baada ya kuzindua Jengo la kutolea huduma ya usafishaji figo lililopo katika hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Joseph – Peramiho. Amesema tabia hiyo inaweza kuhatarisha Maisha ya mwanadamu hususani pale figo iliobaki inaposhindwa kufanya kazi.
Aidha Makamu wa Rais ametoa rai kwa watanzania kujenga tabia ya kupima afya walau mara moja kwa mwaka ili kuepukana na hatari za maradhi kufikia hatua mbaya zaidi. Makamu wa Rais amesema ni vema kuachana na ulaji usiofaa, unywaji wa pombe kupitiliza pamoja na kuhimiza kufanya mazoezi kuepukana na hali hiyo.
Halikadhalika Makamu wa Rais amewataka viongozi na watalaam wa afya kuendelea kutoa elimu ya namna ugonjwa huo unavyopatikana ili kuwasaidia wananchi kuepukana nao.
Makamu wa Rais amesema ugonjwa wa Figo ni miongoni mwa magonjwa yanayoongoza kusababisha vifo vya watu wengi duniani ambapo nchini Tanzania inakadiriwa kuwa kwa kila Watanzania mia moja Watanzania saba wanasumbuliwa na ugonjwa sugu wa figo. Ameeleza kwamba asilimia kumi (10) ya wagonjwa sugu wa figo nchini wamefikia hatua ya mwisho ambayo inahitaji matibabu mbadala ya figo, yaani kusafishwa damu au kupandikizwa figo nyingine.
Makamu wa Rais ameongeza kwamba serikali inatekeleza afua mbalimbali zenye lengo la kuzuia na kudhibiti ugonjwa wa figo na magonjwa mengine yasiyoambukiza ambapo hadi sasa zaidi ya Madaktari bobezi wa figo 20 na zaidi ya Wauguzi bobezi 10 wamehitimu mafunzo na wanatoa huduma kwenye hospitali mbalimbali. Amesema kufikia mwisho wa mwezi Juni, 2023, serikali imefanikiwa kutoa huduma za kusafisha damu kwa wagonjwa takribani 3,500, paamoja na kupandikiza figo kwa wagonjwa 74 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na wagonjwa 33 katika Hospitali ya Kanda ya Kati ya Benjamin Mkapa, Dodoma.
Dkt. Mpango amepongeza Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Joseph – Peramiho kwa kutoa huduma ya kusafisha figo ambayo itakua msaada kwa wananchi wa mkoa huo na maeneo ya Jirani.
Kwa Upande wake Mbunge wa Jimbo la Peramiho na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Jenista Mhagama ameishukuru serikali kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika eneo hilo katika sekta za Afya, Elimu na Miundombinu.
Waziri Mhagama amesema zaidi ya shilingi milioni 400 zimetolewa kwaajili ujenzi wa stendi ya kisasa katika Halmashauri hiyo pamoja na ujenzi wa zahanati katika vijiji 50.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.