Na Albano Midelo,Mbambabay
KAMATI ya Kadumu ya Bunge ya Maji na Mazingira ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mheshimiwa Jackson Kiswaga imeridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maji miwili inayogharimu shilingi bilioni 3.7 wilayani Nyasa mkoani Ruvuma.
Miradi iliyokaguliwa na Kamati hiyo ni mradi wa maji Ngumbo unaogharimu shilingi bilioni 2.5 na mradi wa maji Malungu Kata Tingi unaogharimu shilingi bilioni 1.2.
Akitoa taarifa ya miradi hiyo Meneja wa RUWASA Wilaya ya Nyasa Mhandisi Masudi Samila ameutaja mradi wa maji Ngumbo ulianza kutekelezwa Novemba 2023 na unatarajia kukamilika Aprili 30 mwaka huu ambao utahudumia wakazi Zaidi ya 11,000.
Amezitaja kazi zinazotekelezwa katika mradi huo unaohudumia kata za Ngumbo na Liwundi ni ulazaji wa bomba la maji lenye urefu wa meta Zaidi ya 29,000,ujenzi wa vituo 30 vya kuchotea maji na ujenzi wa tanki lenye ujazo wa lita 200,000 na kwamba mradi umefikia wastani wa asilimia 60.
Akizungumzia mradi wa maji Malungu,Meneja huyo wa RUWASA wilaya ya Nyasa amesema mradi huo unagharimu Zaidi ya shilingi bilioni 1.2 na kwamba utekelezaji wa mradi umefikia Zaidi ya asilimia 80 na unatarajia kuwanufaisha wakazi Zaidi ya 9,000.
Akizungumza baada ya kukagua miradi hiyo kwa nyakati tofauti,Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Marypricsa Mahundi amesema awamu ya pili ya utekelezaji wa mradi huo itaendelea na kwamba mwezi ujao italetwa shilingi milioni 200 kuendelea kutekeleza mradi huo.
Amemwagiza Meneja wa RUWASA wilaya ya Nyasa kumsimamia Mkandarasi kwa kushirikiana na viongozi wa vijiji ili mradi huo uweze kutekelezwa kwa wakati na kuanza kuwahudumia wananchi.
“Ni lazima wananchi tuwasogezee maji nyumbani ili waepukane na adha ya kuamka usiku kufuata maji,nani anataka kuamka usiku wa manane na kufuata maji,akinamama tutunze ndoa zetu,Meneja wa Wilaya haya ni maagizo tekeleza’’,alisisitiza Mhandisi Mahundi.
Amesema Rais Dkt.Samia Suluhu ameagiza kumtua mama ndoo kichwani ambapo amesema mama anatakiwa asitembee umbali wa Zaidi ya meta 400 kufuata maji ili kumwezesha mama kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali na kuongeza kipato.
Naye Mbunge wa Muleba Kaskazini Mheshimiwa Charles Mwijage amesema Rais Dkt.Samia ameokoa Maisha ya wanaume wa Wilaya ya Nyasa kwa kuwasogezea huduma ya maji.
Ametoa rai kwa wanaume kuhakikisha kuwa katika mradi wa maji awamu ya tatu wanaunganisha bomba hadi ndani ya nyumba ili akinamama waweze kupata maji ndani ya nyumba.
“Wanaume tunakufa sana,tatizo mojawapo linalosababisha tufe ni mama akienda kuchota maji mbali,wewe pressure inapanda juu kwa wivu,mama Samia kwa kuwaletea maji amewaokoa’’,alisisitiza Mwijage.
Naye Mbunge wa Jimbo la Nyasa Mhandisi Stella Manyanya ameomba kuongezwa kwa vituo vya kuchotea maji viwe jirani Zaidi na wananchi.
Hata hivyo ameishukuru serikali kwa kutekeleza miradi hiyo ya maji ambayo inakwenda kumaliza changamoto ya maji katika kata za Ngumbo, Liwundi na Tingi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira Mheshimiwa Jackson Kiswaga amesema Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ametoa fedha za kutekeleza miradi ya maji Zaidi ya 1700 katika nchi nzima na kwamba katika Mkoa wa Ruvuma pekee serikali inatekeleza miradi ya maji 36 inayogharimu shilingi bilioni 66.
Ameahidi Kamati hiyo kushughulikia haraka changamoto mbalimbali za miradi ya maji walioikagua na kwamba lengo la serikali ni kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa asilimia 100 ambapo amesema watahakikisha fedha za wakandarasi zinatoka mapema ili waweze kukamilisha miradi hiyo.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.