SERIKALI ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli, imetoa Sh milioni 150 kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa bwalo na jiko, katika shule ya Sekondari ya Kilumba, Kata ya Lumeme Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma.
Akitoa taarifa ya mradi huo kwa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Ruvuma, Kaimu Afisa Elimu Sekondari Halmashari ya Nyasa Oscar Elias amesema, ujenzi wa Mradi huo umetekelezwa kwa kutumia Force account, ambao ulianza Septemba 20, 2019 na kukamilika Desemba 20 ,2019.
“Mradi umetoa ajira za muda kwa watu 60, ikiwa ni wanawake 16 na wanaume 44. Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa na wananchi wa Kata ya Lumeme, tunaishukuru Serikali ya CCM kwa kutekeleza kwa vitendo Ilani ya Chama cha Mapinduzi’’,alisema.
Akizungumza baada ya kukagua Mradi huo, Katibu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Ruvuma Nuru Ngeleja, amesema Kamati ya Siasa ya CCM mkoa, imeridhishwa na utekelezaji wa mradi huo.
Ngeleja amewaomba wananchi siku ya uchaguzi Mkuu kujitokeza kwa wingi na kuwapigia kura Viongozi wa CCM, Kuanzia Rais, Wabunge na Madiwani ili kuwatia moyo ya kuendelea kuwatumikia, katika kipindi kingine cha miaka mitano.
Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT) wa Mkoa wa Ruvuma Kuruthumu Mhagama, amewapongeza wananchi wa Kata ya Lumeme, kwa kujenga bwalo, na bweni la Watoto wa kike katika Shule ya Sekondari Kilumba,ambapo amesema bweni litasaidia kupunguza mimba za utotoni.
Mhagama ameutaja Mkoa wa Ruvuma kuwa ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa mimba za utotoni, Hivyo amewaasa wazazi na walezi, kuwathibiti watoto wao ili kupunguza tatizo hilo na kuwawezesha watoto wa kike kutimiza ndoto zao.
Kwa upande wake Mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa, Musa Homera amesema ili kuonesha Shukrani kwa, Rais John Magufuli,ameshauri kujitokeza kupiga kura nyingi za Ndiyo katika uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu.
“Mimi nataka niwaambieni Shule, Hospitali na Majengo mengine ya Serikali yaliyojengwa Miaka 40 iliyopita, yanalingana na majengo yaliyojengwa kwa fedha za Serikali katika kipindi cha miaka mitano, cha uongozi wa Rais Magufuli”, amesisitiza Homera.
Sera ya Elimu ya mwaka 2014 pamoja na ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015, inaipa kipaumbele sekta ya elimu na itahakikisha Serikali inasimamia sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014.
Imeandaliwa na
Albano Midelo na Netho Credo
Maafisa Habari Serikalini
Mbambabay
Juni 29,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.