KAMATI ya Siasa ya CCM Mkoa wa Ruvuma imewaagiza watendaji na wataalam kusimamia na kuhakikisha miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao kukamilika ndani ya mkataba ili wananchi waweze kunufaika ma miradi hiyo.
Maagizo hayo yametolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma Odo Mwisho wakati kamati hiyo inakagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa nyakati tofauti wilayani Tunduru.
Kamati haijaridhishwa na kutokamilika kwa asilimia 100 kwa miradi ya maji milonde kata ya Matemanga ambayo serikali imetoa zaidi ya shilingi milioni 215 ,kutekeleza mradi huo ambao umefikia asilimia 75,
Mradi mwingine ambao haujakamilika kwa asilimia 100 ni ujenzi wa bwalo la chakula katika shule ya sekondari Nandembo ambao serikali imetoa shilingi milioni 100 kutekeleza mradi huo.
Kamati ya Siasa ya CCM pia haijaridhishwa na kuchelewa kukamilika ujenzi wa bweni lenye uwezo wa kulaza wanafunzi 400 katika sekondari ya wasichana Masonya ambao serikali imetoa zaidi ya shilingi milioni 100 kutekeleza mradi huo.
Akizungumza kwa nyakati tofauti mara baada ya kukagua miradi hiyo,Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma ameagiza mradi wa maji milonde kumalizika kabla ya mwezi Agosti mwaka huu ili kuwaondolea kero ya maji wananchi.
“Hakuna sababu ya kushindwa kukamilisha mradi kwa sababu serikali imeleta fedha za kutosha,hadi sasa mmetumia milioni 44 kati ya milioni 215 zilizopo,huu ni uzembe,alaumiwe nani,DC fanyia kazi tupate taarifa ya mabadiliko kuanzia sasa’’,alisisitiza Mwisho.
Kuhusu bweni la shule ya sekondari ya wasichana Masonya Kamati hiyo imeagiza kuhakikisha bweni linakamilika kwa asilimia 100 na wanafunzi wanaanza kulitumia ambapo ametaka huduma muhimu kama maji,umeme na vitanda na magodoro viwepo.
Amewatahadharisha watalaam kuchukua hatua haraka na kuhakikisha wanafanyakazi na kusimamia miradi kulingana na mikataba na maelekezo yanayotolewa na serikali ili kuwaondolea kero wananchi.
Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro ameahidi kusimamia miradi hiyo ili iweze kukamilika kwa asilimia 100 na kuanza kutoa huduma kwa wananchi ambao wanasubiri kwa hamu.
Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Ruvuma ipo katika ziara ya kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Mkoa wa Ruvuma.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari wa Mkoa wa Ruvuma
Julai 4,2020
Tunduru
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.