BENKI ya NMB imezindua kwa mara ya tatu kampeni ya umebima katika Kanda ya Kusini iliyolenga kutoa elimu ya uwekezaji wa bima na umuhimu wake katika jamii.
Uzinduzi huo umefanyika katika Tawi la NMB Songea mkoani Ruvuma ambapo mgeni rasmi kwenye uzinduzi huo alikuwa ni Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mhe.Michael Mbano.
Akizungumza kabla ya kufanya uzinduzi huo ulioshirikisha wadau mbalimbali wa NMB wakiwemo wafanyabiashara, kampuni mbalimbali za bima,watumishi wa umma na viongozi wa wajasiriamali wadogo(Machinga),Mstahiki Meya Mbano ametoa rai kwa makundi mbalimbali kukata bima ili kukabiliana na majanga mbalimbali.
“Kila mfanyabiashara mdogo awe tayari kukata bima ya biashara yake,NMB wametuanzishia jambo ambalo ni muhimu sana kwa sababu majanga yanatokea muda wowote,hivyo wananchi wote watumie fursa ya bima ya NMB kuwa na uhakika wa Maisha katika biashara zao’’,alisisitiza Mbano.
Amesema wamachinga katika mji wa Songea na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla baadhi yao wanamiliki biashara kubwa hivyo ili kulinda biashara zao wanatakiwa kukata bima ili kuwa na uhakika wa mitaji yao.
Kwa upande wake Meneja wa NMB Kanda ya Kusini Janeth Shango amesema kampeni ya umebima tayari imezinduliwa kitaifa mkoani Mbeya na hivi sasa uzinduzi unfanyika katika ngazi ya Kanda ambapo katika Kanda ya kusini yenye mikoa ya Mtwara,Lindi na Ruvuma uzinduzi umefanyika mjini Songea mkoani Ruvuma.
Amesema licha ya umuhimu wa bima katika Maisha ya kila siku,uchunguzi umebaini bado muitikio wa watu kuweka bima umekuwa mdogo hivyo NMB imeamua kuanzisha kampeni ya umebima ili idadi ya watanzania wanaoweka bima iweze kuongezeka walau kufikia asilimia 50 ifikapo mwaka 2029/2030.
Amesisitiza kuwa kampeni ya umebima inakwenda kutoa elimu ya bima kwa njia mbalimbali ili kuhakikisha watanzania wanaweka bima katika mali,afya au Maisha kwa ujumla ili kuongeza mchango wa sekta hiyo ndogo ya fedha kwenye pato la Taifa.
Ameitaja Benki ya NMB kuwa ndiyo Benki pekee nchini iliyozifikia wilaya zote nchini hivyo inaweza kusaidia upatikanaji wa huduma ya bima katika nchi nzima zikiwemo wilaya zote za Kanda ya Kusini.
“Bima ni kitu muhimu sana na imekuwa msaada mkubwa sana yanapotokea majanga mbalimbali,tujifunze kupitia majanga hayo yakiwemo ya moto hivyo tuendelee kuweka bima,ni muhimu idadi kubwa ya watanzania kujipatia bima’’,alisisitiza Shango.
Naye Mwenyekiti wa Klabu ya Wafanyabiashara Mkoa wa Ruvuma(NMB Bussines Club) Michael West ametoa rai kwa wafanyabiashara wote kujiunga na bima ili kuchukua tahadhari dhidi ya majanga yanayotokana na Maisha.
Salum Masamaki ni Mwenyekiti wa Machinga Mkoa wa Ruvuma ameipongeza NMB kwa kutoa elimu ya kuweka bima kwenye masoko yote mjini Songea hali ambayo amesema itawawezesha wafanyabiashara wadogo kuweka bima kuanzia ngazi ya chini.
Abed Nchimbi ni Mwenyekiti wa Bodaboda Mkoa wa Ruvuma na Salvatory Mangasila Mwenyekiti wa Bajaji Mkoa wa Ruvuma wameipongeza NMB kwa kuleta huduma ya bima ambayo itawawezesha wamiliki wa bodaboda na bajaji ambao wamekopeshwa pikipiki hizo na NMB kuziwekea bima.
Kampeni ya umebima iliyozinduliwa mjini Songea inatarajiwa kufanyika kwa sita mtaa kwa mtaa, nyumba kwa nyumba na duka kwa duka ili kuhakikisha elimu ya umebima inawafikia wananchi wote.
Imeandikwa na Albano Midelo Ruvuma
Februari 20.2023
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.