KANISA la Upendo wa Kristo Masihi-Kiuma,limekabidhi vifaa tiba mbalimbali ambavyo gharama yake haijafahamika mara moja kwa kituo cha afya Mchoteka wilaya ya Tunduru ikiwa ni kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita kuboresha huduma za afya wilayani.
Mganga mfawidhi wa kituo hicho Dkt Theresia Rugemalila,amelishukuru kanisa la Upendo wa Kristo Masihi kwa msaada huo na kueleza kuwa,vifaa hivyo vitaboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi wanaofika kupata matibabu kutoka kata ya Mchoteka na maeneo mengine ya wilaya ya Tunduru.
Dkt Rugemalila alisema, katika kituo hicho mahitaji halisi ya vitanda ni 60 na vilivyopo 27 tu upungufu vitanda 23,kwa hiyo vitanda vilivyotolewa na kanisa vitaongeza nguvu hasa katika wodi ya akina mama na watoto ambako mahitaji yake ni makubwa.
Alisema,tangu kituo cha afya Mchoteka kilipopanuliwa kwa kujengwa majengo mapya,kimekuwa kimbilio la watu wengi kutoka ndani na nje ya kata ya Mchoteka wanaokwenda kupata huduma za afya,kwa hiyo kupatikana kwa vitanda hivyo ni ukombozi mkubwa kwa kuwa vitasaidia kupunguza changamoto na mahitaji ya vitanda.
Amehakikishia Askofu wa kanisa hilo Noel Mbawala kuwa,vifaa hivyo vitatunzwa na vitatumika kuokoa maisha ya Watanzania na kuwaomba wadau wengine kujitokeza kuisaidia Serikali ya katika jitihada zake katika kuboresha huduma za kijamii ikiwemo za afya
Alisema kuwa,serikali iko tayari kushirikiana na madhehebu ya dini na wadau mbalimbali katika kuhakikisha afya za wananchi zinakuwa salama,na kuongeza kuwa milango iko wazi kwa taasisi nyingine za dini zinazotaka kuunga mkono juhudi hizo za serikali ya awamu ya sita.
Kwa upande wake Askofu Mkuu wa kanisa la Upendo wa Kristo Masihi-Kiuma Noel Mbawala alisema,vifaa vilivyotolewa na kanisa hilo ni kutekeleza huduma ya kimwili,kuisaidia jamii na kuwawezesha madaktari na wauguzi kuhudumia wananchi.
Ametaja baadhi ya vifaa vilivyotolewa na kanisa hilo ni vitanda vya kulala watu wazima,vitanda vya kujifungulia na watoto,viti mwendo na kwamba huo ni mwendelezo wa kanisa hilo kusaidia huduma za kijamii katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Askofu Mbawala alisema,kanisa la Upendo wa Kristo Masihi-Kiuma linaamini kwamba ili mtu aweze kumtumikia Mungu ni lazima awe na afya njema,hivyo kupitia msaada wa vifaa tiba wagonjwa watahudumiwa vizuri na kurudi katika hali zao za kawaida kwa kuendelea kumtumikia Mungu na kufanya shughuli zao za maendeleo.
Pia alisema,kanisa la Upendo wa Kristo Masihi limetoa magodoro 20 kwa wafungwa wa gereza la maji maji,wametoa mashine ya kudurufu karatasi(Printer)katika shule ya msingi Milonde na magodoro 20 katika shule ya Sekondari ya Matemanga.
Muuguzi kiongozi wa kituo hicho Baraka Mwakanjemba alisema,ili madaktari na wauguzi waweze kutekeleza majukumu yao vizuri lazima wawezeshwe vifaa,hivyo msaada huo utawaongezea morali na kuwatia moyo katika utendaji wa kufanya kazi.
Alisema,kwa sasa kuna wauguzi wanne ambao wanalazimika kufanya kazi kwa masaa 24 ili wagonjwa wanaofika waweze kupata huduma bora na kuiomba serikali kuviongezea nguvu ya wafanyakazi na vifaa tiba vituo vya afya na zahanati zilizo maeneo ya pembezoni.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.