ZAIDI ya kaya 4,000 katika Halmashauri ya wilaya Tunduru mkoani Ruvuma,zinatarajia kunufaika na fursa ya kilimo cha umwagiliaji kupitia utekelezaji wa mradi wa skimu ya umwagiliaji ya Nambarapi iliyopo kata ya Masonya wilayani humo.
Mradi huo unaotekelezwa na Serikali kupitia Tume ya Taifa ya umwagiliaji,utawanufaisha wakulima wanaolima mazao mbalimbali ikiwemo Mpunga,mahindi pamoja na mazao ya mboga mboga.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo Mhandisi wa umwagiliaji mkoa wa Ruvuma Lusia Chaula alisema,mradi utatekelezwa kwa muda wa siku 560 kuanzia tarehe 15 Julai 2024 na utakamilika tarehe 31 Disemba 2025.
Chaula amezitaja gharama za mradi ni Sh.6,314,477,066.00 na utajengwa kwa kumtumia Mkandarasi kampuni ya M/S Company Ltd JV Otendo ambapo zaidi ya ekari 1,700 zimetengwa kutumika kwenye mradi huo.
Kwa mujibu wa Chaula, kazi zilizopangwa kutekelezwa ni ujenzi wa banio na tuta,ujenzi wa mfereji mkuu mita 5,975,ujenzi wa mfereji wa upili mita 8,825,kujenga mfereji wa matupio,ujenzi wa barabara za mashamba,ujenzi wa vivusha maji na ofisi ya Mhandisi wa mradi
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Tunduru Chiza Marando amesema,haijawahi kutokea katika wilaya hiyo kuwa na mradi wa umwagiliaji wenye thamani kubwa tangu wilaya ilipoanzishwa.
Marando amesema,mradi wa skimu ya umwagiliaji Nambarapi unakwenda kutoa uhakika wa chakula na kupatikana kwa ajira za muda kwa vijana wengi wanaotoka katika kata ya Masonya na wilaya ya Tunduru kwa ujumla.
“kupitia mradi huu tuna mhakikishia Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwamba,wilaya ya Tunduru tutaendelea kuwa na uwezo mkubwa wa kuzalisha na uhakika wa chakula ambacho kinaweza kutosheleza mahitaji ya wananchi wetu”alisema.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru Simon Chacha,amemtaka mkandarasi kuhakikisha anatekeleza mradi huo haraka na kwa viwango kama ilivyo kwenye makubaliano yaliyopo katika mkataba.
Chacha,amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa jitihada anazofanya za kuleta maendeleo katika wilaya ya Tunduru ikiwemo kutoa zaidi ya Sh.bilioni 6.3 fedha ambazo zitatumika kutekeleza mradi huo wa umwagiliaji utakaowanufaisha wananchi wengi hususani wakulima wa wilaya ya Tunduru.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.