Wizara ya Maliasili na Utalii imeunda Kamati ya Kitaifa inayosimamia urejeshwaji wa malikale zilizo nje ya nchi,likiwemo fuvu la Jemedari wa Wangoni Nduna Songea Mbano ambalo limehifadhiwa nchini Ujerumani.
Jemedari wa wangoni Songea Mbano na wenzake mashujaa wa vita ya majimaji 66 walinyongwa na wajerumani mwaka 1906,ambapo wajerumani walikata kichwa cha Songea na kukipeleka nchini Ujerumani ambako kimehifadhiwa hadi sasa.
Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Mambo ya Kale Dkt.Emanuel Bwasiri akizungumza kwenye tamasha la kumbukizi ya mashujaa wa vita ya Majimaji mjini Songea,amesema Kamati ya kitaifa inaendelea vizuri kushughulikia suala hilo ili kuhakikisha malikale zote zilizo nje zinarejeshwa nchini.
“Sisi kama Wizara tunaamini mipango yote iliyowekwa ikienda vizuri,tunatarajia baada ya mwaka mmoja au miwili fuvu la Songea Mbano linaweza kurudishwa hapa nchini’’,alisisitiza.
Hata hivyo amesema fuvu la Songea Mbano litakaporudishwa mawasiliano yatafanyika kati ya wenye fuvu na serikali kuangalia namna fuvu hilo litakavyohifadhiwa hapa nchini.
Akizungumza kwenye kilele cha tamasha la kumbukizi la mashujaa wa vita ya Majimaji,mgeni rasmi Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii mheshimiwa Mary Masanja ameiagiza Kamati ya Kitaifa inayoshughulikia urejeshwaji wa malikale zilizopo nje ya nchi likiwemo fuvu la Songea,kuhakikisha wanatekeleza na kukamilisha kazi hiyo kwa haraka.
Amesisitiza kuwa serikali imedhamiria malikale hizo likiwemo fuvu la Songea Mbano zinarejeshwa hapa nchini na kuzifanya kuwa kumbukizi .
“Naomba kutoa taarifa rasmi kuwa miongoni mwa malikale zilizoshughulikiwa na kuhakikisha zinarejeshwa nchini ni Pamoja na fuvu la Songea Mbano ambaye ni miongoni mashujaa 67 wa vita ya Majimaji waliouwa kwa kunyongwa na wajerumani mwaka 1906’’,alisisitiza.
Amesema kumbukumbu za mashujaa wa vita ya majimaji zinawezesha kizazi cha sasa na kijacho kujifunza namna watanzania walivyojitolea maisha yao katika harakati za ukombozi dhidi ya wakoloni.
Naibu Waziri Masanja pia amekemea vitendo viovu vinavyoendelea kujitokeza katika jamii vinavyoharibu mila,utamaduni na desturi za mtanzania ambapo amewaasa wazazi na walezi kusimamia maadili mema kwa vijana wao.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas akitoa salamu za Mkoa kwenye kilele cha tamasha la kumbukizi la mashujaa wa Majimaji, amelitaja lengo la tamasha hilo kuwa ni kuwambuka mashujaa 67 waliouawa kikatili na wajerumani kwa kunyongwa Februari 27,1906 ambao walizikwa katika eneo ambalo yamejengwa Makumbusho ya Taifa ya Majimaji.
Amesisitiza kuwa tamasha hilo linasaidia kukuza utalii wa utamaduni na kurithisha mila na desturi za mtanzania kupitia matamasha ya utamaduni.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Dkt Noel Lwoga amesema Makumbusho ya Taifa katika kuunga mkono juhudi za Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan inalenga kuifanya jamii kuona umuhimu wa tamasha la Majimaji kwao na kuifanya ishiriki kikamilifu kutangaza mila,utamaduni na desturi zao.
Ameyataja malengo ya tamasha hilo kuwa ni kutambua mchango wa historia ya mapambano ya wananchi dhidi ya ukoloni na kuwaenzi wapiganaji wa vita ya majimaji,kutoa fursa kwa wadau kutembelea na kuona vivutio vya utalii vilivyopo kusini mwa Tanzania hususan mkoani Ruvuma na kuweka mkakati wa kuviendeleza.
Kaulimbiu ya tamasha la kumbukizi la mashujaa wa vita ya majimaji mwaka huu ni makumbusho yetu,urithi wetu kwa maendeleo ya utalii na uchumi.
Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Mkoa wa Ruvuma
Februari 27,2023
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.