Wananchi wa Kijiji cha Luhangarasi, Kitongoji cha Punga katika Wilaya ya Nyasa, Mkoa wa Ruvuma wameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapelekea mradi wa kisima cha maji safi na salama, hatua ambayo imeleta unafuu mkubwa katika maisha yao ya kila siku.
Mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa Programu ya Visima 900 inayosimamiwa na Wizara ya Maji kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), ambapo Wilaya ya Nyasa ni miongoni mwa wilaya zinazofaidika.
Kisima hicho cha Punga tayari kimekamilika na huduma ya maji imeanza kutolewa rasmi kwa wananchi.
Akizungumza kuhusu utekelezaji wa mradi huo, Kaimu Meneja wa RUWASA Wilaya ya Nyasa, Mhandisi Evart alisema mradi huo unahudumia wakazi wapatao 3,498 wa eneo hilo.
Alisema kazi iliyofanyika ni pamoja na uchimbaji wa kisima, ununuzi na ufungaji wa pampu, tanki lenye ujazo wa lita 10,000, vifaa vya ujenzi pamoja na ufungaji wa mfumo wa sola ambapo Jumla ya Shilingi milioni 79.5 zilitumika kutekeleza mradi huo.
Mbunge wa Jimbo la Nyasa, Mhandisi Stella Manyanya, alizindua rasmi mradi huo na kueleza kuwa kwa muda mrefu wananchi wa Kitongoji cha Punga walikuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa ya maji, hivyo kukamilika kwa mradi huo ni ukombozi mkubwa kwao hasa kina mama na watoto waliokuwa wakitembea umbali mrefu kutafuta huduma hiyo muhimu.
Mradi huu wa maji safi na salama si tu umepunguza adha ya upatikanaji wa huduma ya maji, bali pia ni ushahidi wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha maisha ya Watanzania waishio vijijini
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.