Kituo cha Afya Mapera kilichopo Kata ya Mapera, Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kimeanza rasmi kutoa huduma ya upasuaji ikiwa ni mara ya kwanza kwa kituo hicho kutoa huduma hiyo.
Huduma hiyo imeanza kutolewa leo Julai Mosi 2021 ambapo jumla ya akina mama wajawazito watatu wamefanyiwa upasuaji na kufanikiwa kujifungua salama, wawili kati yao wakijifungua watoto wa kike na mmoja akijifungua mtoto wa kiume.
Akizungumzia kuhusu upasuaji huo, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Dkt. Louis Chomboko, ambaye pia ameongoza zoezi hilo amesema upasuaji huo umefanyika kwa mafanikio makubwa na kwamba akinamama wote watatu waliopata huduma hiyo, na watoto waliozaliwa hali zao zinaendelea vizuri.
"Zoezi la leo ni mwanzo tu, ndio tumeanza kutoa huduma hii ambayo itakua endelevu na ambayo itasaidia wananchi wa maeneo haya na maeneo ya jirani kutolazimika kwenda mbali kwa ajili ya kufuata huduma ya upasuaji kwani kwa sasa huduma hiyo inatolewa hapa Mapera". Amesema Dkt. Chomboko.
Aidha, ameongeza kuwa mkakati na mpango wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga ni kuendelea kuboresha na kupanua zaidi huduma za afya katika kituo hicho ikiwemo huduma za Meno na Radiolojia (X-Ray na Ultrasound) ambazo zitaanza kutolewa hivi karibuni.
Ikumbukwe kuwa mwaka 2019 Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga ilipokea fedha shilingi milioni 400 kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya ujenzi wa majengo yanayopewa kipaumbelele ili kuimarisha huduma ya Afya ya Msingi na utoaji wa huduma za rufaa kwenye Kituo cha Afya Mapera, ujenzi ambao ulianza Agosti 2019 na kukamilika Februari 2020.
Miundombinu iliyokamilika kutokana na matumizi ya fedha hizo ni pamoja na Jengo la Upasuaji (Theatre), Jengo la Maabara (Laboratory), Nyumba ya mtumishi inayojitegemea (staff house), Jengo la kufulia nguo (Laundry) na Jengo la Wazazi (Martenity).
Miundombinu mingine ni jengo la kuhifadhia maiti (Mortuary), Kichomeo Taka (Incinerator), Shimo la Kutupia Kondo la nyuma (placenta pit) na Mfumo wa kuvunia maji ya mvua ambayo kukamilika kwa ujenzi huu kumesaidia kuhudumia wakazi zaidi ya 64,000 waliopo Tarafa ya Hagati na meneo mengine ya jirani.
Imeandikwa na
Salum Said,
Afisa Habari, Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.