WANANCHI wa kata Miyangayanga Halmashauri ya mji Mbinga,wameiomba serikali kupitia Halmashauri ya Mji Mbinga kukamilisha ujenzi wa kituo cha afya kilichoanza kujengwa ili kuwaondolea kero ya kwenda hadi Hospitali ya wilaya umbali wa km 7 kufuata matibabu.
Wamesema,kwa muda mrefu wanategemea zahanati ndogo iliyojengwa tangu miaka ya 80 kabla ya kuundwa kwa kata hiyo,ambapo kulikuwa na idadi ndogo ya watu ikilinganishwa na sasa.
Ambudasia Ndunguru mkazi wa Miyangayanga amesema,changamoto katika zahanati hiyo ni kukosekana baadhi ya huduma muhimu ambazo hazitolewa kwenye ngazi ya zahanati ikiwamo upasuaji na watumishi wa kutosha.
Amesema,wagonjwa hasa wajawazito wanapohitaji kujifungua kwa njia ya upasuaji wanalazimika kwenda Hospitali ya wilaya Mbuyula kwa sababu katika zahanati hiyo hakuna vifaa kwa kutolea huduma hiyo.
Richard Komba amesema,hatua ya serikali kupitia Halmashauri ya mji Mbinga kuanza ujenzi wa kituo cha afya ni ukombozi mkubwa kwa wananchi wa kata hiyo kwa kuwa kitakapokamilika kitasaidia kutoa huduma ambazo kwa hazipatikani katika zahanati yao.
Aidha,ameiomba serikali kuhakikisha inakamilisha ujenzi huo haraka ili wananchi waanze kupata huduma karibu na makazi yao badala ya kuendelea kuteseka kwa kutembea umbali mrefu hadi Hospitali ya wilaya au Litembo kufuata matibabu.
Kwa upande wake Mganga Kiongozi wa Zahanati ya Miyangayanga Dkt Revocutus Patrick amesema, wamepokea Sh.milioni 250 kwa ajili ya kujenga kituo hicho cha Afya.
Amesema,matarajio ya wananchi wa Miyangayanga kuwa,kituo hicho kitakapokamilika kitawezesha kupata huduma bora ambazo kwa sasa hazitolewa kwenye ngazi ya zahanati.
Amesema,ujenzi wa kituo cha afya Miyangayanga ulitarajiwa kukamilika tarehe 30 Disemba mwaka 2022,hata hivyo kutokana na changamoto mbalimbali mafundi waliomba kuongezewa muda wa kazi na sasa mradi uko hatua ya kupigwa plasta na utakamilika Mwezi huu.
Amesema, kwa sasa wananchi wengi wanaofika kutibiwa wanasumbuliwa sana na magonjwa ya kifua,malaria na magonjwa mengine na yale ambayo huduma zake hazitolewi kwenye zahanati wanapelekwa kwenye vituo vya afya au Hospitali ya wilaya Mbuyula.
Kwa upande wake Kaimu Afisa mipango wa Halmashauri ya Mji Mbinga Eliud Ngwavi amesema,kituo hicho kitakapo kamilika kitahudumia vijiji vinne vya kata ya Miyangayanga na maeneo mengine jirani.
Amesema,ujenzi ulianza mwezi Oktoba 2022 na unatarajiwa kukamilika mwezi Machi mwaka huu na mpaka sasa majengo matatu ya wagonjwa wa nje (OPD)maabara na jengo la huduma ya mama na mtoto.
Amesema,kwa sasa majengo hayo yako hatua ya kupigwa lipu na yataanza kutoa huduma mara yatakapokamilika rasmi ambapo yakuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wa kata hiyo ambao kwa sasa wanalazimika kwenda vitio vingine kupata huduma ya matibabu.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.