JE WAJUA Rashid Kawawa ndiyo Mcheza filamu wa kwanza Tanzania
MAKUMBUSHO ya Taifa kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii Februari mwaka 2016 ilifanya kumbukizi ya miaka 110 ya mashujaa wa vita vya majimaji na kuenzi mchango mkubwa kwa Taifa wa Waziri Mkuu Mstaafu hayati Rashid Kawawa.
Februari 27 mwaka huu, ni kilele cha kumbukizi ya miaka 117 ya mashuja wa vita ya Majimaji kwa ajili ya kuwakumbuka mashujaa wa vita vya Majimaji 67 waliuawa na wajerumani FEBRUARI 27,1906 .
Waziri Mkuu Mstaafu Hayati Rashid Kawawa ni miongoni mwa mashujaa walipigania uhuru wa Tanzania na kusababisha Uhuru wa Tanganyika kutoka kwa Uingereza kupatikana mwaka 1961 chini ya Rais wa kwanza hayati Mwl.Julius Nyerere.
Mkurugenzi wa Makumbusho ya Taifa ya Majimaji Mhifadhi Barthazar Nyamusya anasema maandalizi ya kufanyika tamasha hilo yanaendelea vizuri yakiwashirikisha wadau wa ndani na nje ya nchi.
Miongoni mwa wadau muhimu katika kumbukizi hilo ni Wizara ya Maliasili na Utalii hususani Idara ya Makumbusho ya Taifa,Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,Baraza la Wazee la Makumbusho ya Majimaji,waandishi wa habari na wadau wengine kutoka Mkoa wa Ruvuma.
Waziri Mkuu Mstaafu hayati Rashid Kawawa pamoja na mambo mengine hawezi kusahaulika katika Nyanja ya filamu Tanzania kwa kuwa alicheza Filamu iliyoitwa Mhogo Mchungu mwaka 1951 ambayo ndiyo Filamu ya kwanza ya Kiafrika Tanzania ambayo ilifuatiwa na filamu nyingine kadhaa ambazo alizicheza na zilijipatia umaarufu mkubwa ndani na nje ya nchi
Kwa mujibu Mhifadhi Kiongozi wa Makumbusho ya Taifa Dar es salaam Philipo Maligisu filamu nyingine ambazo alizicheza hayati Rashid Kawawa ni filamu iliyoitwa meli inakwenda iliochezwa kwa pamoja Kawawa na mkewe Sofia mwaka 1952 mjini Bukoba.
Kulingana na Maligisu,hayati Rashid Kawawa pia alicheza filamu nyingine ambazo zilifungua ukurasa wa filamu Tanganyika ikiwemo iliyochezwa mwaka1953 ilitwa“Wageni Wema” na ilichezwa mjini Arusha na filamu nyingine mbili zilichezwa mwaka1954 moja iliitwa “Chalo Amerudi’ ikifuatiwa na filamu iliyoitwa “Juma Matatani” ilichezwa mkoani Dodoma.
Hivi sasa kuna filamu nyingi za lugha ya Kiswahili ambazo zinatengenezwa na watanzania.Hali hiyo inaonesha uzalendo wa kuendeleza kazi nzuri ya kukienzi Kiswahilias
Wasanii wanaweza kuwa viongozi wazuri wakiingia kwenye siasa,mojawapo ya waigizaji maarufu duniani walioingia kwenye siasa na kuongoza ni Ronald Reagan aliyekuwa Rais wa Marekani kuanzia mwaka 1980 hadi 1988 na Arnold Schwarzenegger aliyekuwa Gavana wa Jimbo la California.
Tanzania ilibahatika kuwa na kiongozi mahiri aliyeanzia kwenye Uigizaji wa Filamu,Waziri Mkuu Mstaafu Rashid Kawawa,shujaa wa kupigania uhuru wa Tanganyika.
Tamasha la kumbukizi ya Vita vya Maji Maji na Utalii wa Utamaduni hufanyika kila mwaka likiwa na lengo la kuwakumbuka mashujaa Watanzania ambao walipigana vita vya Maji Maji na kunyongwa na Wajerumani Februari 27,1906 pamoja na kumuenzi Simba wa vita Hayati Rashid Kawawa.
Mashujaa wapatao 67 walinyongwa mjini Songea mwaka 1906 na walizikwa mahali ambapo sasa imejengwa Makumbusho ya Taifa ya Maji Maji Mahenge mjini Songea.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Makumbusho ya Taifa ya Majimaji Balthazar Nyamusya tamasha hili limekuwa linafanyika kila mwaka kuanzia mwaka 1980 wakati wa ufunguzi wa Makumbusho hiyo, likiwa linasimamiwa na Mamlaka ya Serikali ya Mkoa kwa kushirikiana na Baraza la Mila na Desturi Mkoa wa Ruvuma.
Tangu Mwaka 2010 sherehe hizi zilibadilishwa na kuwa Tamasha la Kumbukizi na Utalii wa Utamaduni baada ya Makumbusho ya MajiMaji kupandisha hadhi na kuwa sehemu ya Makumbusho ya Taifa, chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
Nyamusya anasema tamasha hili hufanyika kila mwaka kwa muda wa siku tatu mfululizo kuanzia Februari 25 hadi Februari 27 ambayo ni siku ya kilele.
“Tamasha lilianza kuratibiwa na Makumbusho ya Taifa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika sekta ya Utalii na Utamaduni, Taasisi za elimu vikiwemo Vyuo Vikuu, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Vyombo vya Habari na Mashirika ya Umma na watu binafsi’’,anasisitiza.
Mhifadhi Kiongozi wa Makumbusho ya Taifa Philipo Maligisu ameyataja malengo ya kufanyika kumbukizi la vita vya majimaji kila mwaka kuwa ni Kutangaza zaidi Tamasha la Utalii wa Utamaduni Ndani na Nje ya nchi ili kuendana na sera ya Utalii ya 2009,sera ya Utamaduni ya 1997 na Sera ya MaliKale ya 2008.
“Sera hizo zinaendana na utekelezaji wa mpango wa nchi wa maendeleo wa miaka mitano,unaoelekeza serikali na taasisi zake kuwekeza zaidi katika utalii na hasa utalii wa utamaduni’’,anasisitiza.
Hata hivyo Maligisu anasema mkazo wa utekelezaji wa sera hizo ni katika maeneo ya kihistoria na kushirikisha nchi zingine kama vile nchi za Jumuiya ya maendeleo kusini mwa Afrika SADDC na nchi ya Ujerumani ambayo inaweza kusaidia kutangaza utalii wa kihistoria.
Anayataja Makusudio na matarajio ya kumbukizi hizo kuwa ni Kutunza kumbukumbu za urithi usioshikika, Kuendeleza utamaduni wa Mtanzania na Kuthamini historia ya nchi na kutunza kumbukumbu za Viongozi wa Kitaifa.
Akimzungumzia Simba wa vita Rashid Kawawa kuingizwa katika kumbukizi za katika Makumbusho ya Taifa,Maligissu anasema ni kutokana na mchango wake katika kuunganisha wafanyakazi wakati wa kupigania uhuru wa nchi pamoja na nchi jirani.
Anasema kupitia kumbukizi hizo wananchi na Taasisi mbalimbali wanapata fursa ya kujifunza na kutathmini juu ya Hayati Rashid Kawawa alivyotoa Mchango wake katika vita vya ukombozi wa Bara la Afrika.
Wasifu wa Waziri Mkuu Mstaafu Rashid Kawawa kwa mujibu wa taarifa za Makumbusho ya Taifa unaonesha kuwa enzi za uhai wake alitoa mchango mkubwa wa kizalendo kwa ajili ya kulitumikia Taifa ikiwemo kuwa Waziri Mkuu mwaka 1962 na kuanzisha Vijiji vya Ujamaa mwaka 1975.
Majukumu mengine ni Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya katiba na mfumo wa Chama kimoja kuanzia mwaka 1964 hadi mwaka 1971,kuwa Waziri wa Ulinzi kuanzia mwaka 1964 hadi mwaka 1980.
Hayati Rashid Kawawa ndiye alianzisha Jeshi la Kujenga Taifa JKT Julai 10 1963,Jeshi la Mgambo 1971,kuwa katibu Mkuu wa Kwanza na Makamu wa Mwenyekiti wa CCM na alianzisha Ujenzi wa Makao Makuu ya Chama mjini Dodoma.
Historia inaonesha kuwa Hayati Kawawa akiwa katika Wizara ya Maliasili na Utalii alianzisha Idara ya Mambo ya kale,uchapishaji nyaraka za kale na kuanzisha Idara ya wanyama pori (Uhifadhi na usimamizi) mwaka 1951,alikuwa Rais wa Shirikisho la Wafanyakazi wa Serikali mwaka 1954 na alikuwa Mbunge kuanzia mwaka 1958 hadi 1985 alipostaafu.
MAKUMBUSHO YA Dkt.RASHID KAWAWA
Tayari katika mji wa Songea kuna Makumbusho ya Dk.Rashid Kawawa.Katika maadhimisho ya kumbikizi za mashujaa wa Vita ya Majimaji iliyofanyika Februari,27,2015 sanjari na onyesho la Historia ya Hayati Dk.Rashid Kawawa katika maadhimisho,familia iliahidi kutoa nyumba moja kubwa ya mbele ya familia pamoja na nyumba nyingine za uwani zilizopo katika eneo la Bombambili mjini Songea.
Nyumba hizo zilitolewa kwa ajili ya Makumbusho ya Rashid Kawawa,lengo kuu ni kuanzisha Makumbusho ya Rashid Kawawa ili kutunza na kuhuisha historia nzuri iliyotukuka ya Hayati Dk.Rashid Kawawa Simba wa vita.
Makumbusho ya Kawawa yalianzishwa rasmi na kufunguliwa Februari 27,2017.
Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma
Februari 22,2023
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.