WAMATENGO WANAVYOENDELEZA UTAMADUNI WAO KUPITIA JIWE LA MBUJI LENYE MAAJABU MENGI
MKOA wa Ruvuma una vivutio vingi tofauti ambavyo bado havitumiki katika kuchangia pato la Taifa na kuinua uchumi wa wananchi wa eneo husika.
Jiwe la Mbuji ambalo lipo katika wilaya ya Mbinga ni miongoni mwa vivutio adimu na vya kipekee vilivyopo katika Bonde la ziwa Nyasa ambalo linajumuisha mikoa ya Mbeya,Ruvuma na Njombe.
Afisa Maliasili na Utalii wa Mkoa wa Ruvuma Africanus Challe anasema tayari Idara yake imeliingiza jiwe la Mbuji kwenye orodha ya vivutio vya utalii katika Mkoa wa Ruvuma ili hatimaye kazi ya kutangaza eneo hilo na vivutio vingine iweze kufanyika kwa tija.
Kivutio cha jiwe la Mbuji kimekuwa gumzo kwa wengi waliosikia taarifa za kivutio hicho.Neno Mbuji kwa lugha ya kabila la wamatengo ni "Kitu kikubwa",jiwe hili lipo katika kijiji cha Mbuji kata ya Mbujii na limekuwa kivutio adimu kwa wageni wa ndani na nje ya nchi.
Jiwe la Mbuji lina maajabu mengi yakiwemo jiwe pekee kubwa Mkoani Ruvuma,Lina vyanzo vingi vya maji chini yake,ni vigumu kulipanda bila kuwaona wazee kwa sababu ni vigumu kupanda na kulizunguka jiwe hilo bila kufuata mila na desturi za kabila la wazee wa kimatengo.
Unapofika katika jiwe hilo inakulazimu kuwatafuta wazee wanaotoa maelekezo kwa yeyote anayetaka kupanda jiwe hilo,ambalo linaheshimika sana na wakazi wanaolizunguka jiwe hilo.
Utafiti umebaini kuwa, sehemu kubwa ya wananchi wanaolizunguka jiwe jiwe la Mbuji hawajawahi kulipanda wala kulisogelea kwa hofu ya kupoteza maisha.
Mzee Sixmund Ndunguru 100 anasema kuwa ili kupanda jiwe hilo ni lazima uwe na Mwongozaji ambaye ni mzee wa mila ambaye anazifahamu vizuri mila na taratibu za kabila la wamatengo zitakazokuwezesha kupanda jiwe hilo bila matatizo na kufurahia vivutio vilivyopo.
“Ninayafahamu maajabu ya jiwe la Mbuji tangu nikiwa na umri wa miaka mitano, mandhari ya jiwe hili hayajabadilika wala kuharibiwa Tangu nilipolifahamu jiwe hili’’, anasema Alex Ndunguru mkazi wa Mbuji.
Kulingana na Ndunguru,mimea adimu ambayo imekuwepo katika jiwe hilo tangu miaka ya 1940 alipopanda juu ya jiwe hilo kwa mara ya kwanza akiwa na baba yake mzazi na kwamba kila mtu anaruhusiwa kupanda jiwe hilo kwa kuzingatia maelekezo ya wazee wa mila na desturi.
Wamatengo wanaamini kuwa katika jiwe hilo kuna viumbe vinavyoitwa Ibuuta ambavyo ni mfano wa binadamu na kwamba viumbe hivyo ni vifupi na vya ajabu ambavyo majira ya usiku vinadaiwa kuonekana.
Hata hivyo viumbe hivyo vifupi vinapatikana katika mataifa mbalimbali ambayo yamekuwa yanapewa majina mbalimbali.
Historia inaonesha kuwa jiwe ka mbuji tangu zamani lilikuwa linatumiwa na wazee kwa ajili ya kutambika katika mila na desturi kwa kufuata mila na desturi ikiwemo kutumia unga wa mhogo na kujipaka kabla ya kuanza kupanda jiwe hilo.
Taratibu hizo sio tu zinatumika kwa ajili ya wenyeji bali hata watalii wageni wanaotaka kupanda jiwe hilo ni lazima watumie unga huo kinyume na hapo mtu anaweza kupata matatizo mengi ikiwemo kupoteza maisha.
“Iwapo mtalii ataamua kupanda jiwe hilo bila kuwaona wazee wa mila na desturi atakuwa amevunja mila na desturi na anastahili kupata adhabu.
Kutokana na maajabu hayo Ndunguru anasema ndiyo maana jiwe hilo linaitwa jiwe la maajabu ambayo yanavutia wengi.
Uchunguzi umebaini kuwa unapoliangalia jiwe la mbuji kwa mbali linaonekana kwamba ni fupi lakini kadri unavyolikaribia ndivyo jiwe hilo linavyoonekana kuwa refu na kuwa na ugumu kulizunguka lote kwa muda mfupi hali ambayo inasababisha watalii wengi wanaotembelea jiwe hilo kuona hayo ni maajabu ambayo yanatakiwa kufanyiwa utafiti zaidi kwa kushirikiana na wazee wa mila.
Ukiliangalia jiwe hilo kwa mbali utaona kama lina kibiongo, na kwamba jiwe hili lina sehemu maalum ya kuanzia safari ya kukwea.
Hata hivyo kinachoshangaza zaidi ufikapo hapo juu Mwonekano wa jiwe hilo hubadilika na hapo unakuta ni kama uwanja wa michezo.
Jiwe la Mbuji pia hutumika kuwaombea watu wanaosumbuliwa na mapepo ambao hupandishwa juu ya jiwe hilo na kuombewa kimila na kwamba inaaminika mapepo hayo huondoka na wagonjwa wa mapepo wanakuwa wamepona kabisa wanaposhuka chini ya jiwe hilo.
Takwimu zinaonesha kuwa kila mwaka idadi ya watalii kutoka ndani na nje ya nchi wamekuwa wanatembelea jiwe hilo ambalo lipo umbali wa kilometa 150 kutoka makao makuu ya mkoa wa Ruvuma mjini Songea.
Leodigar Kumburu(100) mkazi wa Kijiji cha Mbuji anasema wazazi wake kabla ya kusafiri walikuwa wanakwenda kuhiji katika jiwe hilo.
Serikali ya Kijiji cha Mbuji kwa kushirikina na wazee wa mila wameamua kuboresha mazingira ya eneo la kivutio hicho cha utalii kwa kujenga nyumba za mila za wamatengo,kupika vyakula vya asili na ngoma za jadi ili watalii wakishaona jiwe hilo waweze kupata vyakula na ngoma za asili ya wamatengo hivyo wananchi kujipatia kipato.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.