ZIWA Nyasa limezungukwa na nchi tatu ambazo ni Tanzania,Malawi na Msumbiji.Ziwa hilo lipo kwenye usawa wa meta 500 toka usawa wa bahari.
Kulingana na utafiti ambao ulifanywa na jumuiya ya nchi zilizo kusini mwa Afrika(SADC) kwa kushirikiana na nchi ya Uingereza kwenye ziwa Nyasa,ulionesha kuwa ziwa hilo lina kiasi cha tani 165,000 za samaki.
Licha ya kuwa na samaki wa aina mbalimbali,ziwa Nyasa pia lina utajiri wa maliasili nyingine ambazo huwezi kuzipata mahali popote duniani.
Moja ya maliasili asili hizo adimu ambazo zinaweza kukuza uchumi wa watu wa Mwambao mwa ziwa Nyasa ni wadudu ambao wanafahamika kwa jina la likungu ambao wanapatikana kwenye ziwa hilo pekee.
Likungu ni kitoweo ambacho kinatajwa na wataalam wa afya kuwa na utajiri wa protini na madini mengi ya chuma kuliko vyakula vingine hali ambayo inasababisha wananchi wanaokifahamu chakula hiki kukigombania kinapopatikana na kusababisha kuwa na soko kubwa kwa walaji.
Ukibahatika kuona likungu limendaliwa kuwa kitoweo huwezi kutambua kuwa hao ni wadudu mfano wa mbu ambao wametengenezwa kwa ufundi wa hali ya juu badala yake unaweza kudhani ni aina fulani ya nyama au samaki wanaopatikana ziwa Nyasa.
Efonsia Turuka(50) Mkazi wa Kijiji cha Hongi Kata ya Liuli Wilaya ya Nyasa Mkoa wa Ruvuma anasema ameanza kula likungu tangu alipokuwa ana umri wa miaka saba na kwamba kitoweo hicho ni muhimu kiuchumi na kiafya.
“Likungu ni chakula cha asili cha watu wa mwambao mwa ziwa Nyasa kinapendwa na wengi kutokana na kuwa na virutubisho adimu pia kina ladha tamu na kusababisha wengi kupenda kula ingawa upatikanaji wake ni sio wa kila siku.’’, anasisitiza Turuka.
Turuka ni mwanamke ambaye anatengeneza wadudu hao na kuwa kitoweo anasema akinamama wengi mwambao mwa ziwa Nyasa wana ujuzi wa kutengeneza wadudu hao kuwa kitoweo ambacho kinaweza kutumika kwa muda mrefu.
James Chale mkazi wa Liuli anasema wadudu kabla ya kukamatwa nchi kavu na kutengenezwa kitoweo wanaanzia kuruka angani katikati ya ziwa Nyasa kwenye mpaka wa Tanzania na nchi ya Malawi hadi kufika ufukweni mwa ziwa na kutua kwenye miti.
Challe anasema, inaaminika wadudu hao wanaotengeneza likungu wanatoka chini ya ziwa Nyasa na kuibuka juu ya ziwa wakiwa ndani ya mfano wa puto la asili.
“Wakishaibuka juu ya ziwa puto hilo hupasuka na wadudu hao kusambaa hewani kwa mbali wanaonekana mfano wa kimbunga ambacho kinakwenda taratibu kulingana na kasi ya upepo hadi nchi kavu.
Anasema wanawake wakiona hali hiyo wanajiandaa kuwakamata wadudu hao ambao baada ya kufika nchi kavu wanatua kwenye majani ya miti iliyopo jirani na ziwa Nyasa.
Veronika Kamanga mkazi wa Liuli anasema wadudu hao wakitua kwenye majani ya miti akinamama wakiwa na vifaa maalum kama vile vikapu walivyovilowanisha kwa maji wanatumia mianzi kufunga vikapu hivyo na kuanza kuwakusanya wadudu hao ambao wanajaa kwenye vikapu hivyo na baadaye kuwafinyanga na kuwatengeneza katika maumbo tofauti yakiwemo duara au ngumi.
“Mara baada ya likungu kutengenezwa katika umbo la duara akinamama wanazungushia majani ya migomba kisha wanatumia mkaa kuanza kulichoma hadi majani ya mgomba yanapokuwa yameungua yanaashiria kuwa likungu limeiva hivyo wanatoa kwenye mkaa tayari kwa kuliwa’’,anasema.
Hata hivyo anasema likungu hilo kabla ya kuliwa kama kitoweo wakazi wa mwambao wanaunga kwa kutumia karanga,nazi au kuchemsha kwa maji na chumvi.
Likingu ili liweze kusafirisha maeneo ya mbali kutoka ziwa Nyasa,akinamama hao wanaendelea kulikausha kwenye jua ili lisiweze kuharibika na kwamba likungu linaweza kukaa bila kuharibika kwa siku 30.
Likungu mwambao mwa ziwa Nyasa linauzwa kati ya shilingi 1000 hadi 2,000 kutegemeana na ukubwa wake.
Hata hivyo sio jambo rahisi kulikuta likungu sokoni kutokana na watu wengi wanaolijua kununua kwa wingi na kusababisha kuwa na uhaba mkubwa wa upatikanaji wa kitoweo hicho adimu duniani.
Vikta Zambia Mkazi wa Kijiji cha Nkali ziwa Nyasa anasema hadi sasa asili ya likungu haifahamiki vizuri ingawa baadhi ya watu wanadai kuwa ni watoto wa samaki wakubwa.
Zambia anabainisha kuwa katika ziwa Nyasa kuna samaki wakubwa wanaitwa bogobogo ambao ukubwa wa samaki hao unafanana na tumbo la mbuzi mkubwa hivyo inaaminika likungu wanakuwa ndani ya tumbo la samaki hao.
“Samaki hao wanapatikana katikati ya ziwa Nyasa ndiyo wanaowatapika wadudu hao ambao wanaruka hadi nchi kavu na kutua kwenye majani ya miti,baada ya siku tatu wasipookotwa wadudu hao baadhi yao inadaiwa wanarudi tena hadi katikati ya ziwa na kumezwa tena na samaki hao’’,anadai Zambia.
Baadhi ya wavuvi wanaovua samaki aina bogobogo katika ziwa Nyasa akiwemo Martin Challe,John Ndomba na Frank Vumu wamekiri kuwa ukimpasua samaki huyo kwenye tumbo lake unakuta amemeza wadudu hao aina ya likungu.
Hata hivyo wanadai kuwa bado haijathibitika kisanyansi iwapo samaki hao wanaweza kuzaa wadudu kwa kuwa samaki anazaa watoto wa samaki.
Wavuvi hao wanadai kuwa siku ambayo likungu linamwagika katika ziwa Nyasa, samaki wakubwa wanaovuliwa mbali katika ziwa Nyasa hasa aina ya bogobogo,kambale na mbufu wanapatikana kwa wingi hali ambayo inaonesha kuwa kuna uhusiano wa likungu na samaki wakubwa.
Anania Nkomola Mkazi wa Kijiji cha Mkili mwambao mwa ziwa Nyasa anasema likungu ni wadudu ambao wanaibuka kwa kusukumwa na upepo kutoka katikati ya ziwa Nyasa wakiwa mfano wa moshi.
Utafiti unaonesha kuwa likungu ni lishe muhimu inayotengenezwa kwa njia mbalimbali kama vile kuchomwa na kuchemshwa na kwamba unaweza kula likungu likiwa bichi.
Watalaam wa afya wamethibitisha likungu huongeza damu kwa haraka hivyo wakazi wa mwambao mwa ziwa Nyasa ambao wanashambuliwa na malaria,likungu ndiyo lishe muhimu ambayo inawasaidia kukabiliana na tatizo la upungufu wa damu.
Happy Lazaro Muuguzi Mwandamizi na mwenyeji wa Wilaya ya Nyasa Mkoa wa Ruvuma anasema mgonjwa ambaye amepungukiwa damu akitumia likungu katika kipindi cha siku saba damu inarudi katika kiwango cha kawaida.
Anasisitiza kuwa likungu limesaidia kupunguza tatizo la watu wanaokabiliwa na upungufu wa damu mwambao mwa ziwa Nyasa hasa kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano ambao wanashambuliwa zaidi ya ugonjwa wa malaria
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.