Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Antipas Lissu, amekamatwa na Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma kufuatia tuhuma za kutoa matamshi ya uchochezi yanayohusiana na uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2025.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi, tukio hilo limetokea Aprili 9, katika mtaa wa Soko Kuu, Wilaya ya Mbinga, ambapo Lissu anadaiwa kutoa kauli zinazoweza kuashiria kuvuruga mchakato wa uchaguzi huo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, SACP Marco Chilya, amesema kuwa uchunguzi wa tuhuma hizo ulikuwa ukiendelea kwa muda kabla ya hatua ya kumkamata kuchukuliwa rasmi.
“Lissu amehamishiwa jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mahojiano zaidi na maafisa wa upelelezi,” alisema Kamanda Chilya na kuongeza kuwa uchunguzi bado unaendelea ili kubaini iwapo kuna msingi wa kisheria wa kumfikisha mahakamani.
Kamanda huyo ameonya vyama vyote vya siasa na viongozi wao kuwa makini na kauli wanazotoa, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, akibainisha kuwa vyombo vya dola vinafuatilia kwa karibu matamshi ya kisiasa yanayotolewa kwenye mikutano, vyombo vya habari, na mitandao ya kijamii.
Aidha, amewataka wanasiasa kujiepusha na lugha ya kukashifu vyombo vya usalama au serikali kwa ujumla, akisisitiza kuwa kauli za namna hiyo zinaweza kuchochea uvunjifu wa amani na kuhatarisha usalama wa taifa.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.