MKURUGENZI Mtendaji Halmashauri ya Madaba wilayani Songea mkoani Ruvuma Sajidu Idrisa Mohamed amewapongeza wakuu wa shule za Sekondari kwa kuongoza Kimkoa kwa matokeo ya mtihani wa Taifa kidato cha pili na kidato cha nne mwaka 2023.
Sajid ametoa pongezi hizo wakati anazungumza katika kikao cha tathmini ya Elimu katika Halmashauri hiyo kilichojumuisha wakuu wa shule za sekondari ambacho kimefanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri hiyo mjini Madaba.
Halmashauri ya Madaba imekuwa ya kwanza kati ya Halmashauri nane zilizopo mkoani Ruvuma ambazo ni Halmashauri ya Manispaa ya Songea,Halmashauri ya Namtumbo,Tunduru,Nyasa,Halmashauri ya Songea,Mbinga Mji na Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga
Licha ya matokeo hayo Mkurugenzi huyo amekitaka kikao hicho kuweka mikakati ya pamoja ya mwaka 2024 ili kuhakikisha Halmashauri hiyo inaendelea kufanya vizuri katika taaluma.
“Kwa kutumia kikao hiki mnaweza kubadilishana uzoefu na kujifunza kutoka shule ambazo zimefanya vizuri ikiwemo Sekondari ya wasichana Feo,St Monica na Mahanje Sekondari ili tuweze kufanya vizuri zaidi”,alisisitiza Sajidu.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya wasichana ya Feo Jemaida Erenest ameitaja siri ya shule hiyo kufanya vizuri mitihani ya kitaifa ya kidato cha pili na kidato cha nne ni kumaliza mada kwa wakati, kutoa mazoezi ya kutosha,kuwatia moyo walimu na wanafunzi,kutoa motisha kwa walimu pamoja na kufuatilia ratiba zote za walimu.
Naye Makamu Mkuu wa Shule ya St.Monica Florence Mhuwa amezitaja mbinu wanazotumia kufanya vizuri kwenye mitihani ya kitaifa kuwa ni vizuri wanafunzi kuwapa mitihani mingi ya ndani na nje,kufanya tathmini,kuwasimamia wanafunzi katika masomo na kutoa motisha kwa wanafunzi wanaofanya vizuri .
Baadhi ya wakuu wa shule za sekondari katika Halmashauri ya Madaba wakiwa kwenye kikao cha tathmini ya elimu
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.