Katika tukio la kihistoria linaloashiria mwanzo mpya wa huduma bora za maji safi na usafi wa mazingira, Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Mheshimiwa Peres Magiri amezindua rasmi Bodi ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Wilaya ya Nyasa (MBAUWASA). Uzinduzi huo umeambatana na ugawaji wa Sheria Na.5 ya Maji ya mwaka 2019 pamoja na vitendea kazi muhimu kwa wajumbe wa bodi, ikiwa ni ishara ya dhamira thabiti ya Serikali kusogeza huduma karibu na wananchi.
Akizungumza kwa msisitizo na uzito wa kipekee, DC Magiri ametoa mwongozo mkali wa kiuongozi kwa wajumbe wa MBAUWASA, akiwataka kuwa wazalendo, wabunifu, na wenye maono ya mbali ili mamlaka hiyo ijisimamie kwa ufanisi. Alionya kuwa mamlaka isipojiendesha kitaasisi na kifedha, ipo hatarini kufutwa, jambo ambalo hatakubali litokee wakati akiwa kiongozi wa Wilaya hiyo kwa niaba ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mkurugenzi Mtendaji wa MBAUWASA Mhandisi John Guseseka amesema kuwa mamlaka hiyo ilianzishwa rasmi mwaka 2018, ikiwa katika daraja C, na eneo lake la huduma likiwa Kata za Mbamba-Bay, Kilosa, na Mtipwili. Huduma zake zimekuwa zikiwezeshwa na mapato ya ndani pamoja na uwekezaji wa Serikali Kuu katika miundombinu ya maji.
Kwa sasa, Bodi mpya iliyoteuliwa na Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso mnamo Februari 12, 2025, inatarajiwa kudumu hadi Februari 11, 2028, ikiweka kipaumbele katika huduma endelevu za maji kwa wananchi.
Stanley Vumu – Mwenyekiti
Asifiwe Salum – Mwakilishi wa watumiaji wa kawaida
Dkt. John Papalika – Wawakilishi wa wafanyabiashara
Veronica Simba – Mwakilishi wa wanawake
Leslie Kadambe – Mwakilishi wa watumiaji wakubwa
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa na Mkurugenzi wa MBAUWASA – Kwa nyadhifa
“Tunataka kuongeza upatikanaji wa maji kutoka asilimia 68 hadi 85.” — Stanley Vumu, Mwenyekiti MBAUWASA
“Viongozi wa vijiji na vitongoji simamieni elimu ya ulipiaji huduma za maji, msiwe vikwazo.” — Acheni Mwinshehe, Katibu wa CCM Wilaya ya Nyasa
Katika hotuba yake, DC Magiri hakusahau kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, akisisitiza umuhimu wa kumpa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kura za kishindo kwa kazi kubwa ya maendeleo anayoifanya, hususan katika Wilaya ya Nyasa ambako miradi mingi ya kimkakati imetekelezwa.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.