Katika mapambano dhidi ya changamoto ya watoto kuzaliwa na uzito pungufu pamoja na athari za mimba za utotoni, Manispaa ya Songea imeamua kutovumilia tena! Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Wakili Bashir Muhoja, ametangaza mkakati thabiti wa kuhakikisha elimu ya lishe inakuwa silaha ya kweli ya mabadiliko ya kijamii.
"Hatutaweza kuwa na kizazi chenye afya kama hatutoi elimu ya lishe kuanzia ngazi ya familia hadi mashuleni. Ushirikiano wa idara zote ni lazima Afya, Elimu, Kilimo, Ustawi wa Jamii, na Maendeleo ya Jamii – wote tushikamane!" – Mkurugenzi Muhoja
Kwa kushirikiana na idara ya lishe, shule za msingi na sekondari zimeanzisha vilabu vya lishe, ambavyo hadi sasa vimeenea kwa asilimia 72. Vilabu hivi si tu vinatoa elimu ya lishe, bali pia vinakuza bustani za mboga shuleni — wanafunzi wanajifunza, wanapanda, wanavuna, na kula kilicho bora kwa afya yao.
"Bustani hizi shuleni ni zaidi ya mazao, ni bustani za maarifa, afya na mabadiliko ya fikra," anasema Afisa Lishe Robert Sinkamba.
Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026, Manispaa ya Songea imetenga shilingi milioni 80 kwa ajili ya kuimarisha shughuli za lishe. Kaimu Mweka Hazina, Elliassa Urrasa, anathibitisha kuwa bajeti ya mwaka uliopita ilitumika kwa asilimia 100, jambo linaloashiria dhamira ya dhati ya viongozi wa Songea kuweka afya ya jamii mbele.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.