Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Songea Mheshimiwa James Karayemaha amesema Mahakama imedhamiria kusimamia kwa uzito suala la maadili ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua mbalimbali za uwajibikaji kwa maafisa wa Mahakama.
Ameyasema hayo wakati akiwaapisha wajumbe wa Kamati ya Maadili ya Maafisa wa Mahakama ngazi ya Mkoa katika ukumbi wa Manispaa mjini Songea.
Amewakumbusha wajumbe hao kuwa chimbuko la viapo vyao ni kanuni za uendeshaji wa kamati za maadili za maafisa wa Mahakama kwa ngazi ya Mkoa na Wilaya.
"Kiapo hiki kinawafanya wajumbe wawajibike kwa kuwakumbusha kila mmoja kuyazingatia aliyoapa, kwa kumtanguliza Mungu na kutenda haki bila chuki, huba wala upendeleo," alisema Jaji James.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed amewashukuru na kuwapongeza wajumbe wote wa kamati hiyo walioaminiwa na kupewa jukumu hilo kwa ngazi zote.
Ametoa rai kwa wajumbe hao kuendelea kutoa Elimu juu ya uwepo wa kamati na majukumu yake ili kuwasaidia wananchi kuwasilisha malalamiko yao na kufanyiwa kazi.
"Mmeaminika, kazi zenu zinafahamika pia Serikali ya Mkoa na wananchi wana Imani na nyinyi hongereni sana," alisema Kanali Ahmed.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Mary Makondo ameyataja matarajio ya wananchi ni kupata na kuifikia haki kupitia mifumo na Muundo wa Serikali hasa katika Muhimili wa Mahakama.
"Ninaamini watumishi ambao wamepewa dhamana hii wataendelea kulitekeleza jukumu hilo ipasavyo kwa hofu ya Mwenyezi Mungu na hofu ya Katiba na Sheria ya nchi yetu na wakiangalia wananchi wetu wanawategemea sana,"alisema Bi. Mary.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.