ASILIMIA 85 ya wakazi wa mkoa wa Ruvuma na asilimia 75 ya Watanzania wanatajwa kutegemea sekta ya kilimo kuendesha maisha yao ya kila siku.
Hata hivyo idadi hiyo itaongezeka baada ya serikali na wadau mbalimbali kuanza kuwekeza kwenye sekta hiyo kwa kufungua mashamba makubwa na kuanzisha vyuo vya kilimo.
Lengo la uwekezaji huo ni kuongeza uzalishaji wa mazao ili kujipatia kipato na kuongeza idadi ya wataalam watakaotumia maarifa na elimu yao kufundisha kilimo cha kisasa na kwenda kuanzisha mashamba madogo na makubwa yatakayotumika kama mashamba darasa kwa jamii yetu.
Kanisa la Upendo wa Kristo Masihi-Kiuma lililopo katika kijiji cha Milonde kata ya Matemanga wilayani Tunduru limeanzisha chuo cha kilimo na ufugaji ili kuwapatia mafunzo ya kilimo cha kisasa vijana wa Kitanzania.
Mkuu wa chuo hicho Fulko Hyera anasema,chuo cha kilimo na mifugo Kiuma kimeanzishwa na kanisa baada ya kuona kuna uhitaji mkubwa wa jamii ya Watanzania hasa wanaoishi mikoa ya kusini Ruvuma, Lindi na Mtwara.
Anasema,malengo makubwa ya chuo ni kusaidia jamii hususani vijana walioko mtaani ambao wamemaliza elimu ya kidato cha nne na kidato cha sita lakini wako mtaani kwa sababu mbalimbali ikiwemo wazazi kukosa karo ya kuwaendeleza zaidi kielimu au kufanya vibaya katika matokeo ya mitihani ya mwisho ambayo yangewawezesha kuendelea na hatua nyingine.
“tumeona ni bora hawa vijana tuwachukue tuwaweka hapa ili tuwape mafunzo na kuwajengea uwezo wa kuzalisha mazao mbalimbali ambayo yatawasaidia katika biashara na kuwapa ujuzi wa kufuga wanyama na samaki ili kuwapatia kipato kutokana na mahitaji ya uko mtaani”anasema.
Aidha anataja kundi lingine lililokusudiwa katika mpango huo ni vijana waliomaliza vyuo vya ualimu na vyuo vikuu,hata hivyo wamekosa fursa ya kuajiriwa serikalini,lakini kupitia mafunzo hayo vijana wataweza kujiajiri na wengine kufanya biashara za mazao ya kilimo.
“tunapozungumzia kilimo hasa katika mikoa ya kusini vijana wengi wanaona kama ni adhabu,kwa hiyo sisi tunachofanya ni kuwaandaa kisaikolojia kuwa wajasiriamali,tunawapatia mbinu na kuwajengea uwezo ili baadaye waweze kuzalisha kwa wingi kwa kuwa kilimo ni mtaji,kilimo ni biashara,ni kazi kama nyingine”anasema Hyera.
Anasema haikuwa rahisi kuwapata wanafunzi kusoma kozi za kilimo,hata hivyo mwitikio umekuwa mkubwa na kwa mwaka wa kwanza wa masomo 2023/2024 wameanza na vijana 40
Anasema,chuo kinatoa mafunzo kwa miaka mwili na katika mwaka wa kwanza wanajifunza zaidi kilimo cha mboga mboga ambacho wanaangalia mahitaji ya mboga mboga ambazo zinazosaidia sana kuongeza lishe na virutubisho kwenye mwili wa binadamu.
Anasema,katika shamba la kujifunzia kwa vitendo)wameanza kuzalisha kabichi,nyanya,pilipili,bilinganya,karoti,vitunguu na bamia na katika hatua ya kwanza, vijana wanafundishwa namna ya kuandaa shamba,matuta na vitalu nyumba(green House)ambapo kupitia njia hiyo mkulima anaweza kutumia eneo dogo la uzalishaji na akilihudumia vizuri atapata mazao na mapato mengi.
Anasema,hatua ya pili vijana wanafundishwa kutengeneza mbolea ya mboji(asili) ambayo inatengenezwa kwa kutumia mabaki ya mimea,nyasi,mashudu ya alizeti na samadi inayochanganywa na udongo na pia mbolea ya asili ina faida nyingi kwenye uzalishaji ikiwemo kumpunguzia mkulima gharama ambayo upatikanaji wake unahitaji fedha nyingi na kusababisha baadhi ya wakulima kushindwa kumudu gharama.
Kwa mujibu wa Hyera,faida nyingine zinazopatikana kwenye mbolea za asili ni pamoja na mmea kuwa na nguvu na afya wakati wa ukuaji na inapunguza kiwango kikubwa cha sumu kwenye mwili wa binadamu inayotokana na kula vyakula vinavyozalishwa kwa mbolea za viwandani.
Anaeleza kuwa,mwaka wa pili vijana wanafundishwa ufugaji wa wanyama kama kuku wa mayai na nyama,mbuzi na ng’ombe wa maziwa ambayo yatasaidia kuimarisha afya zao na kuwapa mbinu za kutafuta masoko ndani na nje ya wilaya ya Tunduru.
Hyera anasema kuwa,mahitaji ya chakula,nyama,mayai na mboga mboga hayajawahi kwisha tangu dunia ilipoanza lakini watu wanazidi kuongezeka huku uzalishaji unapungua kutokana na mabadiliko ya nchi na kiuchumi.
Anataja mpango mwingine wa chuo ni kuhakikisha wanayaongezea thamani mazao wanayozalisha(food processing) na wameanda jengo maalum litakalotumika kwa ajili ya kuchakata mazao ya chakula na nyama badala ya kuuza yakiwa mazao ghafi
Anasema,wamejipanga kuhakikisha wanazalishaji majira yote ya mwaka ili wateja wao waweze kupata bidhaa kutoka kwenye mashamba yao na Watanzania wafurahie chakula kinachozalishwa kwa kutumia mbolea ya asili kutoka chuo cha kilimo Kiuma.
Anataja faida zilizoanza kupatikana kutoka kwenye mashamba darasa ya chuo ni pamoja na wanachuo kuanza kula vyakula wanavyozalisha wenyewe ambavyo vimesaidia kubadilisha mlo ikilinganishwa na vyuo vingine ambavyo sehemu kubwa yam lo wao ni maharage na wamekuwa walimu kwa watu wengine.
Hata hivyo anataja changamoto katika kutekeleza mradi huo ni kukosekana kwa masoko ya kudumu kwa kuwa jamii inayowazunguka haina uelewa wa kutosha katika matumizi ya mboga mboga na ameishauri jamii kuanza kutumia mboga mboga ili kupunguza tatizo kubwa la utapia mlo.
Amewataka watanzania hasa kutoka mikoa ya kusini,kujiunga na chuo hicho ili waweze kupata elimu na ujuzi ambao utawasaidia kuondokana na umaskini kuanzia ngazi ya familia na jamii kwa ujumla.
Katibu mkuu wa Taasisi ya Kiuma Daniel Malukuta anasema,mwaka 2022 Kanisa liliona ipo haja ya kuanzisha chuo cha kilimo baada ya kuibaini vijana wengi wa wilaya ya Tunduru wanakosa fursa kutokana na vigezo vya udahili wa wanafunzi wanaotakiwa kujiunga na vyuo vya kilimo hapa nchini.
Anaeleza kuwa,katika chuo hicho wanamfundisha mtu kulima hasa mboga mboga na wako mbioni kuanzisha kozi maalum ya ufugaji ambapo jumla ya vijana 40 walijiunga na chuo kwa mwaka wa kwanza wanajengewa uwezo na kupewa ujuzi wa kuzalisha na kufuga.
Anasema,taasisi ya Kiuma inaamini kuanzishwa kwa chuo hicho itakuwa sehemu ya mchango wake kwa jamii ya wana Tunduru na nchi kwa ujumla hasa wanaoishi katika mikoa ya kusini.
“pale tunamfundisha mtu kulima na kuzalisha iwe mazao ya kilimo au mifugo,tumeanza na kulima matunda na mboga mboga na hapo mbeleni tutaanza kufundisha kozi ya ufugaji wa kuku,mbuzi,ng’ombe na samaki”anasema.
“malengo yetu ni kuendelea kuwagusa watanzania wa maeneo ya kusini ambao bado fursa nyingi zinawapita na maisha yao bado yako chini licha ya mikoa hiyo kuwa na rasilimali nyingi ambazo bado hazijatumika ”alisema Malukuta.
Anaeleza kuwa,huo ni mchango mkubwa na wataisaidia serikali katika kuwa kwamua watu wanyonge,kwa sababu sifa ya kujiunga na chuo cha kilimo na mifugo Kiuma kipo kwa ajili ya watu wote wenye akili timamu.
Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Kanisa la Upendo wa Kristo Masihi lenye makao makuu yake katika kijiji cha Milonde wilayani Tunduru Noel Mbawala anasema,chuo hicho kitakuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa mikoa ya kusini ambao kwa muda mrefu walibaki nyuma kielimu na maendeleo.
Anasema,chuo ni kikubwa na kimeanza kufanya vizuri katika kuwafundisha vijana juu ya kilimo cha kisasa kwa kutumia mbolea za asili na pia vijana waliojiunga na chuo hicho mbali na kupata elimu ya kilimo cha kisasa,lakini watapata ujuzi wa kutengeneza mbolea za asili.
Anasema, malengo yao makubwa ni kuifikia jamii ya watanzania ili iweze kunufaika na huduma zinazotolewa na taasisi ya Kiuma na kuisaidia serikali kumaliza tatizo la ajira na kupitia mpango huo,wanatoa ajira kwa baadhi ya vijana wanaomaliza kwenye vyuo vinavyomilikiwa na Kiuma baada ya kuhitimu mafunzo yao.
Mmoja wa wanafunzi wa mwaka wa kwanza katika chuo hicho Asinath Juma,anaiomba serikali kuwasaidia juu ya suala la mikopo kwa vijana wanaotoka katika vyuo vya kilimo ili waweze kupata mitaji na kuendeleza ujuzi waliopata kupitia vyuo vya kilimo.
Anasema,hatua hiyo itawasaidia vijana wengi wanaomaliza kwenye vyuo hivyo kuwa mfano bora kwa jamii kwa kuzalisha na kufungua mashamba ambayo yatatumika kama mashamba darasa kwa watu wanaowazunguka uko mitaani baada ya kumaliza mafunzo yao.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.