MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Philip Mpango amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma na Kamati ya Ulinzi na Usalama kuongeza nguvu ya kudhibiti mifugo mingi inayooingizwa kiholea mkoani humo.
Dkt.Mpango ametoa agizo hilo wakati anazungumza na wananchi wa Kijiji Matomondo Halmashauri ya Songea akiwa katika ziara ya kikazi ya siku tano mkoani Ruvuma.
“Mikoa mingine tumeharibu ndiyo maana wafugaji wengi wamehamia Ruvuma,Mhe.Mkuu wa Mkoa na Kamati yako ya Ulinzi na Usalama ongezeni nguvu kubaini na kudhibiti wanaoingiza kiholea ng’ombe wengi katika Mkoa wa Ruvuma’’,alisema.
Amesema Mkoa wa Ruvuma ambao unaongoza kwa uzalishaji wa chakula nchini,hivi sasa umezidiwa na idadi kubwa ya mifugo inayozidi uwezo wa Mkoa hali ambayo inaathiri shughuli za kilimo.
Makamu wa Rais amewaonya viongozi wote wanaopokea fedha kutoka kwa wafugaji na kuruhusu idadi kubwa ya mifugo kuingia katika Mkoa wa Ruvuma bila kuzingatia sheria na vibali ambapo ameagiza vyombo vya usalama kuanza kuchukua hatua kali ili kukomesha tabia hiyo.
Amesisitiza kuwa ana taarifa za baadhi ya viongozi kwenye vijiji kupokea shilingi 100,000 kwa kila ng’ombe mmoja anayeingia mkoani Ruvuma ambapo amewataka wafugaji kuondoka kwa wakulima na Kwenda kwenye vitalu walivyotengewa na mkoa.
Makamu wa Rais amesisitiza kulinda vyanzo vya maji na kuhakikisha miti rafiki ya mazingira inapandwa kwenye vyanzo vya maji ili viwe endelevu kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Akizungumza baada ya kuweka jiwe la msingi katika mradi wa barabara ya lami ya Matomondo-Mlale yenye urefu wa kilometa 3.5 na barabara ya changarawe yenye urefu wa kilometa 19,Dkt.Mpango ametoa rai kwa madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani Pamoja na wananchi kuitunza barabara hiyo ambayo serikali imetoa shilingi bilioni nne kutekeleza mradi huo.
Amewaagiza TARURA kusimamia ubora wa barabara hiyo ili iweze kujengwa katika kiwango ili wananchi wapate barabara bora.
Mbunge wa Jimbo la Peramiho Mheshimiwa Jenista Mhagama ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kujenga barabara hiyo ambapo ameiomba serikali kujenga barabara ya lami kuanzia Kijiji cha Matomondo hadi Kizuka kwa kuwa barabara hiyo ni muhimu kiuchumi na kiulinzi.
Makamu wa Rais yupo mkoani Ruvuma kwa ziara ya kikazi ya siku tano kuanzia Julai 20,2023 hadi Julai 24,2023.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.