Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema Kampeni ya Kitaifa ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia inapaswa kuangazia changamoto zinazowagusa wananchi wa hadhi zote wakiwemo watu wenye ulemavu na wanaofanyiwa ukatili wa kijinsia.
Makamu wa Rais amesema hayo leo tarehe 22 Julai 2023 wakati akizindua Kampeni ya Kitaifa ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaign) kwa mkoa wa Ruvuma, uzinduzi uliofanyika katika Uwanja wa Majimaji uliopo Songea mkoani humo.
Amesema kumekuwepo na ongezeko la vitendo vya ukatili wa kijinsia hapa nchini ambapo takwimu za Januari – Disemba 2022 zinaonesha matukio ya ukatili yaliyokuwa mengi zaidi ni ubakaji ambayo ni 6,335, ulawiti 1,555 na mimba za utoto 1,557.
Ametoa wito kwa Kampeni hiyo kusaidia waathirika wa vitendo hivyo kupata haki zao pamoja na kuagiza vyombo vya dola kuendelea kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya watuhumiwa wote wa matukio hayo.
Halikadhalika Makamu wa Rais amesema Kampeni hiyo inapaswa kutoa elimu ya kutosha kuhusu taratibu za kufuata ili kutekeleza Hukumu za Mahakama na kupata haki kwani hivi sasa kumekuwepo na wananchi ambao wameshinda kesi mahakamani lakini wamebaki na hukumu zao mikononi bila kupata haki zao.
Aidha Makamu wa Rais ametoa wito kwa Watanzania kujijengea utamaduni wa kuandika wosia mapema ili kuepusha migogoro ya kifamilia inayotokea pindi mwanafamilia mmoja anapofariki. Amesema kumekuwepo na migogoro mingi ya mirathi inayotokana na watu wengi kutokuandika wosia wakiwa hai hali inayochangiwa na imani miongoni mwa jamii kuwa kuandika wosia ni kujitabiria kifo.
Ameilekeza Wizara ya Katiba na Sheria na Ofisi ya Kabidhi Wasii Mkuu kuongeza jitihada za kutoa elimu kuhusu uandaaji wa wosia na masuala ya mirathi kwa ujumla.
Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama, kudhibiti hali ya uingizaji wa mifugo kinyume na sheria inayoendelea katika mkoa wa Ruvuma hususani Wilaya ya Tunduru, Namtumbo na Songea Vijijini. Amesema kumekuwepo na taarifa ya uingizwaji mifugo inayofanywa na viongozi pamoja na baadhi ya matajiri wa mifugo kutoka nchi jirani ambao wanatoa fedha ili waweze kuingiza mifugo hiyo.
Makamu wa Rais ameitaka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Wizara ya Ardhi kufanya kazi ya dharura kutenga na kupima vitalu na mashamba ya mifugo na wamiliki wa mifugo watakiwe kujenga malambo ya maji katika vitalu na mashamba hayo.
Vilevile Makamu wa Rais ameigiza Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuongeza kasi ya upimaji na upangaji wa miji ikiwa ni pamoja na kurasimisha makazi ya wananchi kwa kuzingatia sheria. Amesema Sekta ya ardhi imeendelea kukabiliwa na migogoro mingi ikiwa kwa sehemu kubwa migogoro hiyo inachangiwa na maeneo mengi kutopimwa na kupangiwa matumizi sahihi pamoja na baadhi ya wananchi kuvamia maeneo ya hifadhi na shoroba za wanyama.
Makamu wa Rais amevitaka vyombo vinavyosimamia sheria ikiwemo jeshi la polisi na Ofisi ya Mashtaka ya Taifa kuzingatia sheria katika utekelezaji wa majukumu yao. Amesema kumekuwepo na malalamiko ya wananchi wengi yanahusu ukiukwaji wa haki za watumiwa ikiwemo kukamatwa bila kufuata taratibu, kunyimwa dhamana kinyume cha sheria, kupekuliwa bila kufuata taratibu, rushwa na kukaa mahabusu muda mrefu bila kufunguliwa mashitaka.
Makamu wa Rais amesema Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia inapaswa kutoa kipaumbele katika kutoa elimu kuhusu haki za watu wenye ulemavu. ameilekeza Wizara ya Katiba na Sheria kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kutoa elimu kwa jamii na kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Watu enye Ulemavu Na. 9 ya mwaka 2010.
Kwa upande wake Waziri wa Katiba wa Sheria Dkt. Damas Ndumbaro amesema Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ni mkakati unaotekeleza maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wenye lengo la kuongeza uelewa wa sheria na haki za binadamu kwa wananchi wote hususani wanawake,watoto na makundi maalum.
Dkt. Ndumbaro ameongeza kwamba Kampeni hiyo itasaidia kuimarisha huduma za ushauri na msaada wa kisheria hususani kwa wananchi wanaoishi maeneo ya pembezoni mwa nchi. Amesema kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia itapita katika kila wilaya, kata, kitongoji, taasisi mbalimbali kama vile za elimu pamoja na maeneo ya vizuizi ikiwemo mahabusu na magereza.
Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Campaign) inatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia Machi, 2023 hadi Februari, 2026 ikitarajiwa kuwafikia katika Mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar. Mkoa wa Ruvuma ni mkoa wa nne kuzindua kampeni hiyo ukitanguliwa na mikoa ya Dodoma, Manyara na Shinyanga.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.