Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amesema Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt.Philipo Isdory Mpango anatarajia kuanza ziara ya kikazi mkoani Ruvuma kuanzia Julai 20,2023 hadi Julai 24,2023.
Akizungumza na wanahabari ofisini kwake mjini Songea Kanali Thomas amesema Julai 20,2023 majira ya 5.00 asubuhi Mheshimiwa Makamu wa Rais anatarajia kuwasili katika Kijiji cha Lilondo Halmashauri ya Madaba na kupokewa na viongozi wa Chama na Serikali kisha kuwasalimu wananchi.
Amesema Makamu wa Rais akiwa katika Halmashauri ya Madaba pia atasalimiana na wananchi Kijiji cha Mlilayoyo kisha kuondoka kuelekea Ikulu Ndogo mjini Songea.
“Mheshimiwa Makamu wa Rais akiwa Ikulu Ndogo Songea atapokea taarifa ya shughuli za maendeleo ya Mkoa wa Ruvuma Pamoja na kukabidhiwa taarifa ya Mkoa ya kazi za Chama Cha Mapinduzi’’,alisema.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mheshimiwa Makamu wa Rais Julai 21,2023 ataanza ziara yake katika Manispaa ya Songea ambapo atazindua kituo cha Afya Lilambo na kuwasalimia wananchi.
Amebainisha zaidi kuwa Mheshimiwa Makamu wa Rais ataondoka Lilambo na kuelekea katika Kijiji cha Matomondo Halmashauri ya wilaya ya Songea ambako ataweka jiwe la msingi,Barabara ya kiwango cha lami ya Matomondo hadi Mlale JKT yenye urefu wa kilometa 4.5,kisha atasalimiana na wananchi na kuelekea hospitali ya Peramiho ambako atafungua jengo la kusafishia figo na kukagua jengo la upasuaji na kusalimiana na wananchi.
Kulingana na Mkuu wa Mkoa,ziara ya Makamu wa Rais mkoani Ruvuma itaendelea Julai 22,2023 kwa Mheshimiwa Makamu wa Rais kushiriki katika kuzindua kampeni ya kitaifa ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaign) katika uwanja wa Majimaji mjini Songea.
Kampeni hiyo inatarajia kufanyika kwa siku kumi kisha kuendelea hadi Desemba 2023.Kampeni hiyo inatarajia kufanyika katika Halmashauri zote nane za Mkoa wa Ruvuma ambapo kila Halmashauri kampeni itafanyika katika kata kumi
Hata hivyo amesema baada ya uzinduzi huo Mheshimiwa Makamu wa Rais atakwenda Kata ya Mwengemshindo Manispaa ya Songea kukagua ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa na kuzindua jengo la mionzi la hospitali ya Rufaa ya Mkoa.
Kanali Thomas amebainisha kuwa Julai 23,2023 Mheshimiwa Makamu wa Rais ataendelea na ziara yake mkoani Ruvuma kwa kutembelea wilaya za Mbinga na Nyasa na kwamba akiwa wilayani Mbinga katika Kijiji cha Kigonsera,Makamu wa Rais atasalimiana na wananchi wa Kigonsera na kisha Kwenda Mbinga mjini ambako atasalimiana na wananchi wa Mbinga mjini.
Amesema Makamu wa Rais ataondoka mjini Mbinga na kuelekea mji Mdogo wa Mbambabay wilayani Nyasa ambako anatasalimiana na wananchi kisha kuondoka na kuelekea Kijiji cha Liuli ambako ataweka jiwe la msingi katika mradi wa maji safi Liuli na kusalimiana na wananchi wa Liuli.
“Natoa rai kwa wananchi wote kujitokeza kwa wingi katika maeneo yote ambayo Makamu wa Rais atapata fursa ya kuwasalimia wananchi’’,alisema.
Mheshimiwa Makamu wa Rais anatarajia kukamilisha ziara yake mkoani Ruvuma Jumatatu Asubuhi Julai 24,2023.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.