WANAFUNZI wa shule ya Sekondari Makita Halmashauri ya mji Mbinga mkoani Ruvuma,wameishukuru serikali kuwajengea vyumba vipya vya madarasa na kupunguza msongamano mkubwa wa wanafunzi madarasani hivyo kuwasaidia kusoma katika mazingira mazuri.
Wamesema,wamefurahishwa na mpango wa serikali ya awamu ya sita kutokana na mkakati wake wa kuboresha na kuweka mazingira mazuri ya kujifunzia kwa wanafunzi na walimu kufundishia ikiwamo vyumba vipya vya madarasa,meza,viti na ofisi za walimu.
Pius Komba mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule hiyo amesema,kutokana na uwekezaji huo wa serikali watahakikisha wanasoma kwa bidii na kufanya vyema katika masomo yao na hatimaye waweze kutimiza malengo yaliyowaleta shuleni.
Komba,amewaomba wazazi ambao bado hawajapeleka watoto wao shule,kuhakikisha wanawapeleka haraka ili wakapate haki yao ya elimu kwani muda wa masomo umeshaanza na wao wamebaki nyumbani.
Aidha,amemshukuru Mkuu wa shule hiyo Mwalimu Emanuel Mwamasika kwa kukubali kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza hata wale wasiokuwa na mahitaji muhimu jambo linalowapa hamasa ya kusoma kwa bidii.
Happy Kinyunyu amesema,madarasa mapya yaliyojengwa kwa ubora yanawafanya wanafunzi kupenda shule,kusoma kwa bidii na kuwa wasikivu darasani ikilinganishwa na hapo awali kwa kuwa hakuna changamoto zinazoweza kuwakatisha tamaa.
Amewaasa wanafunzi wenzake wa kike,kusoma kwa bidii ili kutimiza malengo yao badala ya kujiingiza katika ulevi,uesharati na kufanya kazi za nyumbani(House Girls) tabia iliyopelekea baadhi ya watoto wa kike kushindwa kutumiza malengo yao.
Kwa upande wake Mkuu wa shule hiyo Emanuel Mwamasika amesema,walipokea kiasi cha Sh.milioni 40 ambazo zimefanikisha kujenga vyumba vipya viwili vya madarasa.
Amesema hapo awali kulikuwa na uhaba mkubwa wa madarasa,lakini baada ya kupata fedha hizo na kujenga vyumba vipya sasa wanafunzi wanakaa madarasani kwa nafasi na hakuna aliyekosa meza na kiti na wana ziada ya chumba kimoja.
Mwamasika,ameipongeza serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kutekeleza kwa vitendo Ilani yake jambo lililosaidia kuwa na mazingira mazuri na rafiki katika sekta ya elimu hapa nchini.
Mwamasika amesema,shule hiyo imepangiwa kupokea wanafunzi 332 wa kidato cha kwanza na hadi kufikia tarehe 4 wiki iliyopita wanafunzi walioripoti ni 220 sawa na asilimia 96.4.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.