CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeungana na Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan kuipa pole familia ya Hayati Ngoyai Edward Lowasa na wanachama wote wa chama huku kikieleza kuwa Tanzania imepoteza kiongozi mwema ambaye ametoa mchango mkubwa katika taifa katika nafasi zote za uongozi alizohudumu.
Salamu hizo za pole zilitolewa leo na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Paul Makonda wakati akihutubia wananchi wa wilaya ya Songea Mjini mkoani Ruvuma ukiwa ni muendelezo wa ziara yake ya mikoa 20.
“Mpendwa, kiongozi wetu, na mwanachama wetu wa Chama cha Mapinduzi aliyekuwa Waziri Mkuu Mstaafu Mheshimiwa Lowassa amefariki leo Februari 10 saa nane mchana katika hospitali ya Moyo pale Muhimbili,”
“Chama cha Mapinduzi kiunaungana na Mwenyekiti wetu na Watanzania wote, kuipa pole familia ya Hayati Ngoyai Edward Lowassa na wanachama wa Chama cha Mapinduzi na kumuomba Mungu kwa kudra zake atupe uvumilivu katika wakati huu mgumu wa msiba ambao wanachama wa Chama cha Mapinduzi kwa kumpoteza mwanachama na familia kumpoteza baba, mjomba na babu” Amesema Makonda.
Amesema kwa niaba ya CCM wanatoa pole kwa wanachama na wapenzi wa chama hicho,wakereketwa na Watanzania wote kwa ujumla kwa kuwa Lowasa alikuwa kiongozi mwema na kwa nafasi zake zote alitoa mchango mkubwa katika taifa hili.
Makonda amesema Hayati Lowassa atakumbukwa kwa mambo mengi lakini pia kwa umahiri wake wa kujenga hoja katika nyakati tofauti na kufanya kazi katika taifa hili lakini kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu hawana budi kukubaliana na kazi ya Mungu.
Amesema wakati anaanza ziara yake alifanikiwa kupita katika Jimbo la Monduli na kuongelea mema yake kwasababu wote walikuwa kwenye Chama hicho.
“Wakati tunaanza ziara yetu, Dar es Salaam, tukaenda Pwani, tukaenda Tanga, Kilimanjaro, na tulipofika Arusha tulipata nafasi ya kwenda kwenye Jimbo la Monduli, kaka yangu Fredy Lowasa akiwa ndiyo Mbunge, na tulimkumbuka Mzee wetu kwasababu wote tumekuwa kwenye chama hiki na katika utumishi wa serikali tukiwafahamu viongozi wetu, Hatukujua ya kwamba kabla ya kumaliza ziara yetu tutapata taarifa nzito na ngumu kama hizi lakini yote ni mapenzi ya Mungu,”amesema.
Amesema kutokana na Rais Samia kutangaza maombolezo na kushusha bendera nusu mlingoti kwa siku tano, wao kama Chama wanajipanga kusubiri utaratibu ili wanachama wote waweze kujulishana namna watakavyoshiriki katika kumuhifadhi katika nyumba yake ya milele.
“Mheshimiwa Rais ametangaza maombolezo na kushusha bendera kwa siku tano, kupitia tangazo hilo la kiongozi wetu na Mwenyekiti wetu wa chama, na sisi kama chama tutajipanga kusubiri utaratibu ili wanachama wote tuweze kujulishana hatua na namna tutakavyoshiriki katika kumuhifadhi katika nyumba yake ya milele, mengi tutayapa na mengi tutayasema kadri ya ratiba na viongozi wetu Wakuu wanavyotuelekeze” Amesema.
Hayati Waziri Mkuu mstaafu, Lowassa amefariki Jana saa nane mchana wakati akupatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Mrisho Kikwete (JKCI).
Lowassa alihudumu kama Waziri Mkuu wa Tanzania chini ya Rais wa awamu ya nne ya Rais mstaafu, Jakaya Kikwete kwa miaka mitatu, toka 2005 mpaka 2008.
Lowassa alizaliwa Agosti 26, 1953 na amefariki akiwa na umri wa miaka 70
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.