Utalii wa kiutamaduni hapa nchini bado haujapewa kipaumbele ukilinganisha na nchi nyingine kama Afrika ya kusini ambayo utalii huo umepiga hatua kubwa.
Mkoa wa Ruvuma una utajiri mkubwa wa utalii wa utamaduni ukilinganisha utalii wa ikolojia,miongoni mwa vivutio vya utalii wa utamaduni ni Makumbusho ya Taifa ya Majimaji yaliopo katika eneo la Mahenge Manispaa ya Songea.
Afisa Maliasili na Utalii wa Mkoa wa Ruvuma Afrikanus Challe anabainisha kuwa,wadau wa utalii katika Mkoa wa Ruvuma wamekusudia kuanzisha na kukuza utalii wa kiutamaduni (cultural tourism) sanjari na kuboresha maeneo yote ya kihistoria ili kuendeleza utamaduni hatimaye maeneo hayo yaweze kuingiza mapato baada ya watalii kutembelea kama ilivyo katika visiwa vya Zanzibar.
Challe anasema,wadau wa utalii mkoani Ruvuma tayari wameshatembelea maeneo muhimu ya kihistoria kama vile Makumbusho ya Taifa ya Majimaji,Makumbusho ya Rashid Kawawa,Maposeni,Luhira,Peramiho na Chandamali katika Wilaya ya Songea ili kutambua maeneo ya kihistoria na umuhimu wake kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.
“Huu ni mwanzo wa jukumu la kuziboresha kumbukumbu za kihistoria katika mkoa wa Ruvuma na kuimarisha utalii wa ndani na nje lengo likiwa ni kuutangaza mkoa wa Ruvuma’’,anasisitiza Challe.
Kwa upande wake Mhifadhi Kiongozi wa Makumbusho ya Taifa ya Majimaji Bartazar Nyamusya anasema serikali imedhamiria kuyafanya Makumbusho ya Taifa ya mashujaa wa vita ya Majimaji kuwa makumbusho ya mfano Tanzania kutokana na makumbusho hayo kuhifadhi vifaa halisi na silaha halisi ambazo walitumia mashujaa hao kupambana na wakoloni wa kijerumani.
“Hii ni Makumbusho pekee nchini iliyoanzishwa mwaka 1980 ambayo imebahatika kuwa na vifaa vyote asilia na muhimu katika utamaduni na historia ya mtanzania hali ambayo inaitofautisha makumbusho hii na nyingine zilizopo hapa nchini ”,anasisitiza Mhifadhi huyo.
Naye Mhifadhi Kiongozi wa Makumbusho ya Taifa Philipo Maligisu anabainisha zaidi kuwa Mji wa Songea ni miongoni mwa miji michache nchini ambayo ilitoa upinzani mkali katika vita ya Majimaji na kwamba katika makumbusho hayo kuna ushahidi ambao unaonesha moja kwa moja kuwa wazee wa Songea walishiriki kikamilifu katika vita hivyo.
Anabainisha zaidi kuwa katika eneo la mashujaa wa majimaji yamejengwa majengo mbalimbali ambayo yamehifadhiwa vifaa ambavyo ni mila na utamaduni wetu vilitumiwa na mashujaa hao ili kuwaletea watanzania uhuru.
Maligisu anasema ndani ya Makumbusho ya Taifa ya Majimaji kuna mnara wa kumbukumbu ya wanajeshi ambao walitoka Songea kwenda kupigana vita ya Idd Amini kati ya mwaka 1978 hadi 1979 ambapo wakati wanarudi baada ya kushinda vita hiyo walipata ajali mbaya na kufariki dunia askari wote 56 katika milima ya Lukumbulu wilayani Songea.
Amesema Ili kuwakumbuka mashujaa hao serikali ilijenga mnara katika eneo Makumbusho ya Taifa ya Majimaji ambako walizikwa mashujaa wa vita ya majimaji kama sehemu ya kuwakumbuka hivyo kurithisha mila,ushujaa na utamaduni wa mtanzania.
Kulingana na sera ya utamaduni ya mwaka 1997 pamoja na sheria ambayo inayatambua maeneo haya serikali imeamua mji wa Songea uingizwe katika vivutio vya utalii wa kiutamaduni kwa ajili ya kuendeleza historia ya Mji wa Songea ili uwe wa kihistoria, kishujaa na kiutamaduni.
Utafiti uliofanywa na Makumbusho ya Taifa umebaini kuwa mji wa Songea una vigezo vyote vya kuingizwa katika rasilimali za kiutamaduni za taifa,ili kuhakikisha kuwa watalii wengi wa ndani na nje ya nchi wanafika katika makumbusho hayo ili kujifunza utamaduni wa mtanzania.
Hali ya mila,utamaduni na desturi iliyopo kwa vijana wa sasa katika nchi yetu ni mbaya kwa kuwa vijana wengi wamesahau utamaduni mila na desturi za mtanzania na kuendekeza mila za kigeni ambazo zimeharibu kabisa maadili mema ya mtanzania.
Mbunge Jimbo la Nyasa Injinia Stella Manyanya anasema uhamasishaji wa kufufua utalii wa kiutamaduni kusini unaendelea ili kuhakikisha watu wa rika zote wanatembelea vivutio mbalimbali za utalii ikiwemo Makumbusho ya Taifa ya Majimaji.
Injinia Manyanya ameipongeza Idara ya Makumbusho ya Taifa ya Majimaji kwa kuandika barua kwa wakuu wa shule katika mkoa wa Ruvuma ili kuhakikisha wanafunzi wanapata nafasi ya kutembelea vivutio vya utalii na kujifunza mambo mbalimbali ili kupenda utalii tangu wakiwa wadogo.
Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasilino Serikalini ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma
Januari 19,2023
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.