Meneja Uchimbaji wa kampuni ya Mgodi wa Makaa ya Mawe ya JITEGEMEE Wilayani Mbinga Mkoani Ruvuma Bosco Mabena amesema malori zaidi ya 120 hubeba makaa ya mawe kwa siku katika mgodi huo na kwamba uzalishaji wa madini hayo unafanyika kwa njia za kisasa.
Mabena amesema hayo wakati anatoa taarifa ya uchimbaji madini ya makaa ya mawe kwa viongozi kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ambao wapo mkoani Ruvuma kwenye kampeni ya kuhamasisha uwekezaji wa ndani na usajiri wa biashara TIC.
Amesema makaa ya mawe yanayozalishwa kwenye mgodi wa Kampuni ya JITEGEMEE hutumika katika viwanda vilivyopo ndani ya nchi,Afrika Mashariki na nchi za Ulaya na China.
“Huu ni mgodi wa kitanzania ambao unaendeshwa na wazawa kwa asilimia 100,tunavyo vitalu vya makaa ya mawe ambavyo vinachimba makaa ya mawe kwa njia ya kisasa kwa sababu tuna vifaa vya kisasa vikiwemo maabara ya kisasa na mitambo ya kuchakata makaa ya mawe kwa ubora wa hali ya juu’’,alisisitiza Mabena.
Amesema makaa ya mawe yanatumika katika viwanda mbalimbali vikiwemo vya saruji katika mikoa mbalimbali nchini,pia amesema makaa ya mawe yanatumika katika viwanda vya tires,nondo na viwanda vyote vidogo vidogo vikiwemo viwanda vya nguo ambapo amesema wanapakia makaa ya mawe bandari ya nchi kavu zaidi ya 120 kwa siku.
Hata hivyo amesema Kampuni ya JITEGEMEE ina ghala la kutunzia makaa ya mawe katika bandari ya Mtwara lenye uwezo wa kutunza makaa ya mawe zaidi ya tani laki tano kwa ajili ya kuuza katika masoko ya nje ya nchi kupitia bandari ya Mtwara.
Kwa upande wake Meneja Uhamasishaji Uwekezaji wa Ndani Kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Felix John ameipongeza Kampuni ya JITEGEMEE kwa uwekezaji mkubwa ambapo amesema TIC imefika mkoani Ruvuma kwa lengo la kutembelea miradi ya uwekezaji wa wazawa katika Mkoa wa Ruvuma iliyosajiriwa kupitia TIC.
Amesema TIC ipo mkoani Ruvuma kwa lengo la kutoa elimu ya uwekezaji wa ndani na usajiri wa miradi katika kituo cha TIC ambapo amesisitiza kuwa wanaamini wananchi wa Mkoa wa Ruvuma watajitokeza kwa wingi kusajiri miradi yao ili waweze kunufaika na vivutio vya kikodi na visivyo vya kikodi vinavyotolewa na serikali kupitia TIC.
Kwa upande wake Afisa Biashara wa Mkoa wa Ruvuma Joseph Kabaro amesema bado Mkoa una fursa nyingi za uwekezaji katika sekta ya madini kwa kuwa Mkoa wa Ruvuma umebarikiwa kuwa na aina mbalimbali za madini.
Ameyataja madini hayo kuwa ni makaa ya mawe,dhahabu,chuma,uranium,madini ya vito, shaba na madini ya ujenzi ambapo amesema hadi sasa kampuni zilizojitokeza kuchumba makaa ya mawe ni 18.
Madini ya Makaa ya mawe katika Mkoa wa Ruvuma yanachimbwa katika wilaya za Songea,Mbinga,Nyasa na Namtumbo.
Kituo cha Uwekezaji Tanzania katika Mkoa wa Ruvuma kimeweza kuwatembelea wawekezaji wazawa wawili ambao ni Kampuni ya SUPEFEO ya mjini Songea na Kampuni ya Uchimbaji madini ya JITEGEMEE wilayani Mbinga.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.