Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za mauaji ya kikatili yaliyogubika Wilaya za Namtumbo na Mbinga, likiwemo tukio la kusikitisha la mama mmoja kuwaua watoto watatu kwa kuwachinja shingoni kwa kutumia kitu chenye ncha kali, tukio linalodaiwa kuchochewa na wivu wa mapenzi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 25, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Marco Chilya, amesema tukio la kwanza lililotikisa jamii lilitokea Julai 12, 2025 majira ya saa 8 mchana katika Kijiji cha Milonji, Kata ya Lusewa, Wilaya ya Namtumbo ambapo mwanamke aitwaye Wende Luchagula (30), mkazi wa kijiji hicho, alituhumiwa kuwaua watoto wa mke mwenzake kwa kuwachinja shingoni.
Kamanda Chilya alieleza kuwa watoto waliouawa ni Lugola Samweli (6), na mapacha wawili, Kulwa Samweli na Doto Samweli, wote wa umri wa miezi 8. Alisema inadaiwa kuwa mtuhumiwa, akiwa na wivu wa mapenzi baada ya kugundua mume wake anampendelea zaidi mke mdogo na watoto wake, alisubiri mpaka mume wake na mke huyo mdogo walipoenda mnadani ndipo akatekeleza mauaji hayo ya kikatili dhidi ya watoto hao wasio na hatia.
Kwa mujibu wa Kamanda Chilya, uchunguzi wa awali umebaini kuwa mtuhumiwa alitumia kisu kuwachinja watoto hao katika mazingira ya kutisha. Miili ya marehemu ilikabidhiwa kwa familia kwa ajili ya maziko, huku mtuhumiwa akiwa mikononi mwa Polisi kwa hatua zaidi za kisheria.
Katika tukio jingine lililotokea Julai 17, 2025 majira ya saa 2 asubuhi katika Kijiji cha Lihale, Kata ya Mkako, Wilaya ya Mbinga, mkazi wa kijiji hicho, Adam Mkinga Chengula (68), aliuawa kikatili na ndugu zake wawili kwa kile kinachodaiwa kuwa ni imani za kishirikina. Kamanda Chilya amesema marehemu alikutwa ameuawa ndani ya zizi la mbuzi nyumbani kwake baada ya kunaswa na kunyongwa na ndugu zake waliotajwa kuwa ni Dastan Mkinga, mkazi wa Bombambili Songea Mjini na Leyson Mkinga, mkazi wa Ruhuwiko Songea Mjini.
Kamanda amesema baada ya tukio hilo, Jeshi la Polisi lilianzisha msako mkali na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa Leyson Mkinga Julai 24, 2025 katika eneo la Ruhuwiko, huku juhudi za kumtia nguvuni mtuhumiwa wa pili, Dastan Mkinga, zikiendelea kwa kasi.
Katika hatua nyingine, Kamanda Chilya ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa wanandoa wanaoridhia kuishi kwenye ndoa za wake zaidi ya mmoja kuhakikisha wanajenga moyo wa uvumilivu, maelewano na kuacha wivu wa mapenzi wa kupindukia. “Endapo kutatokea migogoro ya kindoa, ni busara kutafuta suluhisho kwa njia ya amani kwa kushirikisha viongozi wa dini, wazee au wataalamu wa ushauri wa ndoa,” amesema.
Matukio haya mawili ya mauaji si tu yamezua taharuki kwa wakazi wa Ruvuma, bali pia yameibua mjadala mpana kuhusu athari za wivu wa mapenzi na imani potofu katika jamii. Jeshi la Polisi limeahidi kuendelea na msako wa watuhumiwa waliobaki na kuhakikisha haki inapatikana kwa wahanga wote wa matukio haya.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.