Kambi ya Wapigania Uhuru ya Muhukuru, Wilaya ya Songea, Mkoa wa Ruvuma – Tanzania
Katika picha ya kihistoria isiyofutika kirahisi katika kumbukumbu za Bara la Afrika, marais watatu mashuhuri—Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania, Samora Machel wa Msumbiji na Kenneth Kaunda wa Zambia—walikutana katika Kambi ya Muhukuru, iliyoko wilayani Songea, mkoani Ruvuma.
Hii haikuwa tu ziara ya kawaida. Ilikuwa ni mkutano wa mashujaa wa Afrika, walioungwa mkono na dhamira ya dhati ya kuikomboa Afrika kutoka katika makucha ya ukoloni na ubaguzi wa rangi.
Wakati huo, Kambi ya Muhukuru ilikuwa makazi ya zaidi ya wakimbizi 12,000 waliokimbia mateso ya kikoloni kutoka nchi za Kusini mwa Afrika.
RUVUMA – NGOME YA MAPAMBANO YA UKOMBOZI
Kwa mujibu wa Philipo Maligisu, Mhifadhi Kiongozi kutoka Makumbusho ya Taifa, Mkoa wa Ruvuma unashikilia rekodi ya kipekee kama mkoa uliokuwa na kambi nyingi zaidi za wapigania uhuru nchini Tanzania. Zaidi ya wapigania uhuru 84,000 kutoka nchi kama Msumbiji, Zimbabwe, Angola, Namibia, Afrika Kusini na Zambia walihifadhiwa, kufundwa na kusaidiwa mkoani hapa.
Muhukuru ilikuwa shule ya mapambano, chuo cha uzalendo, na chemchemi ya mshikamano wa Kiafrika. Kupitia kambi hii na nyingine kama Lundo,Likuyu na Masonya, Tanzania chini ya uongozi wa Mwalimu Nyerere, ilitoa mchango mkubwa katika kufanikisha uhuru wa mataifa jirani.
KUMBUKUMBU YA KUINUA VIZAZI
Tukio la kukutana kwa marais hawa watatu halikuwa la kawaida. Ilikuwa ni ujumbe wa mshikamano, matumaini na uthibitisho kuwa Afrika inaweza kujikomboa yenyewe kwa mshikamano.
Picha hii ya kihistoria ni kielelezo hai cha mshikamano wa Afrika. Ni wakati wa kuenzi, kujifunza, na kuendeleza historia za mashujaa waliopigania uhuru wetu kwa damu na jasho.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.