Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma imeweka rekodi mpya ya kiutendaji kwa kuvuka lengo la ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kiwango kikubwa.
Halmashauri hiyo imefanikisha makusanyo ya Shilingi bilioni 12.2 dhidi ya lengo la Shilingi bilioni 8.4 kufikia Juni 30, 2025.
Mafanikio haya yametajwa katika kikao maalum cha Baraza la Madiwani cha kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kilichofanyika hivi karibuni.
Mkuu wa Kitengo cha Fedha na Uhasibu wa Halmashauri hiyo, CPA Samwel Marwa, amesema mapato hayo yameongezeka kutoka Shilingi bilioni 3.4 mwaka 2021 hadi bilioni 12.4 mwaka huu, akibainisha kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya mshikamano wa wataalamu wa Halmashauri, madiwani na wananchi.
Alisisitiza kuwa usimamizi madhubuti wa sheria ndogo pamoja na kuziba mianya ya upotevu wa mapato kumechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko hilo.
CPA Marwa ametaja vyanzo vikuu vya mapato kuwa ni ushuru wa zao la kahawa (Sh. bilioni 4.3), makaa ya mawe (Sh. bilioni 3.3), ushuru wa huduma (Sh. bilioni 1.35), pamoja na ushuru wa mazao na michango kutoka kwa wananchi katika ngazi ya kata.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Mary Makondo, ameipongeza Halmashauri hiyo kwa kupata hati safi kwa mwaka wa fedha 2023/2024, ikiwa ni mara ya nne mfululizo.
Amesema hati safi ni ishara ya usimamizi mzuri wa fedha za umma na utekelezaji wa majukumu kwa kuzingatia sheria na taratibu za Serikali.
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Mkoa wa Ruvuma, Nicolas Kilinga, amehimiza uongozi wa Halmashauri hiyo kujibu kwa wakati hoja zote za ukaguzi ili kudhibiti ongezeko la hoja mpya. .
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.