Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma inatarajia kujenga shule maalumu ya bweni itakayohudumia watoto wenye ulemavu na wanaohitaji uangalizi maalumu.
Akizungumza kwenye kikao cha kujadilia changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Juma Mnwele,amesema shule hiyo inayokusudia kuhudumia watoto wote wenye mahitaji maalumu na itajengwa katika Kata ya Maguu.
Amesema ujenzi wa shule hiyo unatarajia kugharimu shilingi Milioni 250 katika kwa awamu na kwamba kuanzia Julai Mosi mwaka huu Halmashauri hiyo inatarajia kutumia shilingi Milioni 100 ambazo tayari zimetengwa kwenye mpango wa bajeti wa mwaka 2021/2022 kwa ajili ya kujenga madarasa mawili, vyoo na bweni katika shule hiyo.
“katika kuhakikisha azma ya kujenga shule hiyo inatimia, tayari Ofisi yangu imepanga ziara ya wajumbe wa Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango ya Halmashauri ambao watatembelea Kata ya Maguu na kukagua eneo la ujenzi wa shule hiyo kabla ya mwisho wa mwezi huu’’,alisema.
Kwa upande wake Afisa Elimu Maalumu katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Happy Mpete amesema serikali imekua ikichukua jitihada mbalimbali kusaidia jamii ya watoto wenye ulemavu .
Amezitaja jitihada hizo kuwa ni kuajiri walimu wenye elimu maalumu,kujenga miundombinu rafiki kwa wenye mahitaji maalumu na kuweka vitengo maalumu kwa watoto wenye ulemavu hususani wasioona,viziwi na watoto wenye ulemavu wa akili.
Mgeni rasmi kwenye kikao hicho Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Cosmas Nshenye amesema serikali inakusudia kufanya utambuzi wa watu wenye ulemavu kuanzia ngazi ya chini utakaokuza na kuongeza takwimu za uandikishaji wa shule kwa watoto wenye ulemavu.
Hata hivyo amesema uandikishaji kwa wenye ulemavu unahitaji ushirikiano na uwajibikaji wa pamoja baina ya familia, jamii na serikali na kwamba wajibu wa kwanza unaanza ngazi ya familia.
Kujengwa kwa shule hiyo kutaifanya wilaya ya Mbinga kuwa na shule tatu maalumu, Shule mbili za awali ni Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mbinga Girls na Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Mbinga Boys.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Aprili 18,2021
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.