HALMASHAURI ya Mji wa Mbinga Mkoani Ruvuma, imetumia zaidi ya shilingi bilioni tatu zilizotolewa na serikali kwa ajili ya kutekeleza mradi wa jengo la ofisi ya Halmashauri ya Mji na nyumba saba za wakuu wa Idara.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Grace Quintine amesema Halmashauri yake katika kipindi cha mwaka 2019/2020 ilipokea kiasi cha sh.milioni 350 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba saba za wakuu wa Idara ambazo ujenzi wake umekamilika.
“Mradi huu wa nyumba za watumishi utasaidia sana wakuu wa Idara,badala ya Halmashauri kuwalipia pango la nyumba,tutakuwa tumewasaidia nyumba hizi,mradi umefanyika kwa force account na Msimamizi Mkuu wa mradi alikuwa ni TARURA’’,alisema Quintine.
Amesema serikali ya Awamu ya Tano pia imetoa zaidi ya shilingi bilioni 2.9 ambazo zimetumika kutekeleza mradi wa jengo la Halmashauri ya Mji wa Mbinga ambalo limeanza kutumika hivyo kuboresha mazingira ya kufanyia kazi kwa watumishi na wananchi.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme kwa niaba ya wananchi wa Mbinga,amemshukuru Rais Dkt John Magufuli kwa kuruhusu kiasi hicho cha mabilioni ya fedha yaliyowezesha kujengwa jengo bora la Halmashauri ya Mji wa Mbinga na nyumba saba za watumishi.
“Tuna kila sababu ya kumshukuru Rais wetu kwa zawadi hii kubwa,kwa niaba ya serikali nawapongeza wana Mbinga Mji kwa kupata jengo hili zuri na rafiki la kutolea huduma’’,alisisitiza Mndeme.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari wa Mkoa wa Ruvuma
Oktoba 16,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.