HALMASHAURI ya wilaya Mbinga mkoani Ruvuma,imetumia Sh.milioni 500 kutoka mapato ya ndani kujenga kituo cha afya Matiri kata ya Matiri ikiwa ni utekelezaji wa mkakati wake wa kusogeza na kuimarisha huduma za afya kwa jamii.
Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo George Mhina amesema,fedha hizo zimetumika kwa ajili ya kujenga majengo matano ambayo ni jengo la wagonjwa wa nje(OPD)maabara,jengo la wazazi, jengo la kufulia na kichomea taka ambalo ujenzi wake utaanza hivi karibuni.
Amesema,ujenzi wa majengo hayo umekamilika kwa asilimia zaidi ya 90 na Halmashauri imepanga kuanza kutoa huduma angalau za awali mapema mwezi April.
Mhina amesema,kwa sasa kazi inayofanyika ni kutambua watumishi watakaokwenda kufanya kazi katika kituo hicho,kuleta madawa na vifaa tiba pamoja na usajili wake.
Amesema,Halmashauri ya wilaya Mbinga kupitia mapato yake ya ndani imejipanga kuhakikisha vijiji na kata zote kuna vituo vya kisasa vya kutolea huduma ili wananchi ambao ndiyo wanufaika wanafurahia na kwenda kwenye vituo vya serikali kupata huduma mbalimbali za matibabu.
Mkazi wa kijiji cha Matiri Joseph Ndunguru amesema, kujengwa kwa kituo hicho cha afya ni ukombozi mkubwa kwao kwani sasa wanategemea zahanati ndogo ambayo kutokana na idadi ya watu waliopo inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo baadhi ya dawa,vifaa tiba na watumishi.
Nduguru ameiomba serikali,kupeleka vifaa ili ujenzi ukamilike haraka na waweze kupata huduma zote za matibabu karibu, badala ya kuendelea kufuata baadhi ya huduma Hospitali ya wilaya Mbinga kilomita 50 na Hospitali ya St Joseph Peramiho iliyopo umbali wa km 100.
Kwa upande wake fundi anayejenga kituo cha afya Matiri Juma Kombo amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha zinazotumika kujenga na kuimarisha huduma za afya nchini.
Kombo,amewaasa mafundi wenzake wanaopata kazi za kujenga miradi mbalimbali ya maendeleo kuwa waaminifu wa fedha zinazotolewa na serikali ili iendelee kuwaamini mafundi wazawa katika ujenzi wa miradi ya maendeleo nchini.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.