Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga imeweka wazi milango ya uwekezaji kwa kutangaza fursa mbalimbali za kiuchumi zinazopatikana na kukaribisha watanzania kuchangamkia haraka fursa hizo kwa kuwekeza ndani ya Halmashauri hiyo.
Hayo yabebainishwa wakati wa kikao cha Baraza la Biashara la Wilaya kilichofanyika Mbinga Mjini Aprili 17, ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, Juma Mnwele amesema Halmashauri hiyo ina utajiri wa fursa za kiuchumi na kutoa rai kwa mtu yeyote mwenye nia na dhamira ya kuwekeza basi kufanya hima kuja kuwekeza Mbinga.
Mkurugenzi huyo Mtendaji amebainisha kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga ina maeneo mengi ya wazi, makubwa na mazuri ya uwekezaji kwa kufanyika shughuli na fursa mbalimbali kama Viwanda vya kusindika unga wenye virutubisho (Unga Lishe), vituo vya kuuzia mafuta (Petrol Stations), uchimbaji wa makaa ya mawe, uwekezaji kwenye kilimo cha mazao mbalimbali ya biashara kama parachichi, korosho, alizeti, soya, ufuta, na mengineyo ambayo kulingana na tafiti za hali ya udongo yanaelezwa kustawi vizuri kwenye maeneo mengi ndani ya Halmashauri hiyo.
Amesema anakaribisha na kuhamasisha wawekezaji kuja kwa wingi kuwekeza ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kwani Halmashauri hiyo imeweka mazingira yote rafiki na salama kwa uwekezaji ikiwemo kurahisisha upatikanaji wa ardhi na maeneo ya uwekezaji pamoja na uwepo wa miundombinu na huduma muhimu kama umeme, maji na barabara huku akitolea mfano eneo la Kiamili na miji mingine midogo ya Maguu, Matiri, Kigonsera, Ruanda na Mkako ambayo tayari yameshapimwa na kutengwa maeneo maalumu kwa ajili ya uwekezaji.
Akizungumzia kuhusu fursa za uwekezaji zilizopo Kiamili, ambako ni Makao Makuu ya Halmashauri, Mkurugenzi Mnwele amesema kwa sasa Halmashauri hiyo inatekeleza mradi wa ujenzi wa jengo la Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji na ujenzi wa stendi ya mabasi na kwamba anatoa hamasa na kuwakaribisha wadau wa uwekezaji kuchangamkia fursa zilizopo ndani ya eneo hilo, akitolea mfano kuwekeza kwenye ujenzi wa vibanda zaidi ya 200 vya biashara vitakavyojengwa kuzunguka eneo la stendi kwa kuingia ubia na Halmashauri hiyo.
Kikao cha Baraza la Biashara Wilayani Mbinga kimefanyika na kuongozwa na Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Mhe. Cosmas Nshenye na kuhudhuriwa na viongozi, wafanya biashara na wadau wa biashara kutoka Halmashauri zote mbili za Wilaya ya Mbinga ambazo ni Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga na Halmashauri ya Mji wa Mbinga.
Imeandikwa na Salum Said
Afisa Habari Mbinga
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.