HALMASHAURI ya wilaya Mbinga mkoani Ruvuma,katika kipindi cha miezi mitatu Julai hadi Septemba 2024 imekusanya zaidi ya Sh.bilioni 2,964,142,561 sawa na asilimia 35 kati ya lengo la kukusanya Sh.bilioni 8,400,000,000 kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato ya ndani kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Andrew Mbunda amesema hayo ,kwenye kikao cha robo ya kwanza cha Baraza la madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo.
Amesema ,hadi tarehe 30 Septemba Halmashauri imepokea Sh.bilioni 7,042,293,300 sawa na asilimia 26 ya makisio ya Sh.bilioni 27,227,634,000.00 kwa ajili ya mishahara ya watumishi na Sh.bilioni 1,769,097,000 kati ya Sh.bilioni 2,536,195,000.00kwa ajili ya matumizi mengineyo.
Amesema ,ongezeko hilo ni baada ya kupokea Sh.bilioni 1,417,962,000.00 kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajia kufanyika tarehe 27 Novemba kwa ajili ya kuwapata viongozi wa vitongoji na vijiji.
Mbunda amesema, Halmashauri imepokea jumla ya Sh.bilioni 3,291,768,549 kati ya Sh.bilioni 9,918,358,720 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali yenye lengo la kuboresha huduma za kijamii na kuharakisha maendeleo ya wananchi waliopo katika Halmashauri hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Mbinga Mheshimiwa Kisale Makori,amewapongeza watumishi na madiwani wa Halmashauri ya wilaya Mbinga kwa kazi nzuri ya kutekeleza miradi na kusimamia shughuli za maendeleo ikiwemo zoezi la uandikishaji wananchi katika Daftari la wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za mitaa.
Makori aliyewakilishwa na kaimu Katibu tawala wa wilaya hiyo Karim Mzee,amewataka wazazi na walezi kuhakikisha wanachangia chakula kwa ajili ya watoto wao waliopo shuleni badala ya kazi ya kutoa chakula kuachwa ifanywe na Serikali.
Naye Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Amandus Chilumba,amewaomba madiwani kudumisha upendo na mshikamano utakaosaidia Halmashauri yao kuendelea kuwa kinara kwenye makusanyo ya mapato ya ndani katika mkoa wa Ruvuma.
Alisema,Halmashauri itapata maendeleo iwapo kutakuwa na maelewano kati ya madiwani,wakuu wa idara na watumishi wa ngazi ya chini ambao kimsingi ndiyo wanaotumika katika kukusanya mapato na kutekeleza miradi ya maendeleo.
Chilumba,amewataka watumishi na madiwani wa Halmashauri hiyo kubuni na kutafuta vyanzo vipya vya mapato pamoja na kudhibiti mianya yote inayochangia kutoroshwa mapato yanayokusanywa kutoka kwenye vyanzo mbalimbali.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.