Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, amesema kuwa mbio za mwenge mkoani Ruvuma zitaanza tarehe 9 Mei, 2025 ambapo mwenge huo utapokelewa katika Kijiji cha Igawisenga, Halmashauri ya Wilaya ya Madaba, ukitokea Mkoani Njombe.
Akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake, Kanali Ahmed amesema ni muhimu kwa wananchi wa mkoa wa Ruvuma kufahamu kuwa mwenge huo utakimbizwa katika halmashauri zote nane za mkoa wa Ruvuma.
Ametaja ratiba ya mbio hizo katika mkoa wa Ruvuma ambapo Mei 9, 2025 ni Madaba DC, Mei 10, 2025 Songea DC, Mei 11, 2025 Mbinga DC, Mei 12, 2025 Nyasa DC, Mei 13, 2025 Mbinga TC, Mei 14, 2025 Songea MC, Mei 15, 2025 Namtumbo DC, Mei 16, 2025 Tunduru DC na tarehe 17 Mei 2025 mwenge huo utakabidhiwa mkoa wa Mtwara.
Kanali Ahmed ameeleza kuwa pamoja na mambo mengine, kutakuwa na midahalo mbalimbali inayogusa maendeleo na maisha ya wananchi. Amehimiza wananchi wa Ruvuma, wadau wa maendeleo, sekta za umma na binafsi kujitokeza kushiriki mbio hizo na kutumia fursa hiyo kutangaza na kuonyesha shughuli zao kupitia sehemu za mikesha ambazo zitakuwa zimeandaliwa.
Mbio hizo kwa mwaka huu zinaongozwa na kauli mbiu inayohusu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 ambayo inasema "Jitokeze Kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 kwa Amani na Utulivu," kauli mbiu hiyo inaambatana na ujumbe wa kudumu wa mapambano dhidi ya Malaria unaosema "Zero Malaria inaanza na mimi, wewe na sisi wote."
Kauli mbiu zingine ni "Kataa dawa za kulevya, timiza malengo yako," "Kuzuia rushwa ni jukumu langu na lako, tutimize wajibu wetu," na ujumbe unaohusu lishe unaosema "Afya ni mtaji wako, zingatia unachokula."
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.