MBUNGE wa Jimbo la Tunduru Kaskazini Mkoani Ruvuma Hassan Kungu,amewataka viongozi wa Dini wilayani humo,kushirikiana na serikali kuwa elimisha waumini wao kujiandaa kushiriki kuhesabiwa katika zoezi la sensa ya watu na makazi itakayofanyika Mwezi Agosti mwaka huu.
Kungu alisema wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Nampungu kata ya Nampungu akiwa katika ziara ya kukagua na kuhimiza shughuli mbalimbali za maendeleo zinazofanywa na wananchi kwa kushirikiana na Serikali.
Alisema, kuna umuhimu mkubwa kwa viongozi wa Dini kushiriki katika zoezi hilo kwa kuhamasisha wananchi kushiriki vyema kuhesabiwa kwani wanakutana na kuongea na wananchi wengi mara kwa mara ikilinganisha na viongozi Serikali.
Alisema,sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 wilaya hiyo haikufanya vizuri kutokana na baadhi ya viongozi wa dini kupitia nyumba za ibada kuwaeleza waumini wao wasishiriki zoezi hilo kutokana na sababu zao, hivyo serikali ilishindwa kupata taarifa sahihi ya idadi ya watu waliopo.
Kwa mujibu wake,changamoto hiyo kwa kiasi kikubwa imesababisha wilaya ya Tunduru kutopata Halmashauri nyingine, licha ya kuwa na eneo kubwa na watu wengi ikilinganisha na mkoa jirani wa Mtwara.
Kungu,amewahimiza viongozi wa serikali katika ngazi mbalimbali kuhakikisha wanaelimisha wananchi umuhimu wa kushiriki katika sensa, kwa kutoa taarifa muhimu za kaya zao kwani itasaidia Serikali kuwa na taarifa sahihi na kupanga mambo mbalimbali ya mendeleo.
Aidha,amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa makarani watakaopita kwenye makazi yao kuwahesabu kwa kutoa takwimu sahihi na kuepuka kuficha baadhi ya taarifa muhimu kama idadi ya watu na mifugo.
“Ndugu zangu mwakani nchi yetu inatarajia kufanya zoezi la sensa ya watu na makazi,nawaombeni sana sana tushiriki kikamilifu kwa kutoa taarifa sahihi za kaya zetu,sisi Tunduru hatukufanya vizuri katika zoezi la sensa ya watu na makazi iliyopita,serikali haiwezi kuleta maendeleo mahali ambako hakuna taarifa na idadi sahihi ya watu, sasa hivi tunapambana kupata Halmashauri ya pili,lakini haiwezi kutupatia kama idadi ya watu haitakuwa kubwa”alisema.
Pia akiwa katika kijiji hicho,alikagua mradi wa ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa vinavyojengwa kupitia fedha za Maendeleo na ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Covid-19 katika shule ya sekondari Nampungu na kutoridhishwa na kasi ya ujenzi huo.
Hivyo,amewaagiza mafundi na watendaji waliopewa dhamana ya kusimamia mradi wa ujenzi huo,kufanya kazi usiku na mchana na ukamilike haraka ili watoto waliochaguliwa kuingia kidato cha kwanza mwakani wayatumie madarasa hayo.
Wananchi wa kijiji hicho, wamempongeza Mbunge Kungu kutokana na jitihada mbalimbali za maendeleo anazofanya kwani katika kipindi cha mwaka mmoja tangu alipochaguliwa wilaya ya Tunduru imefanikiwa kupata miradi mingi ambayo imepunguza na kumaliza baadhi ya kero.
Hata hivyo,wananchi hao wamemuomba Mbunge Kungu, awasaidie kuwaondoa baadhi ya watumishi wa kijiji hicho ambao wanahusika kuhujumu fedha na miradi mbalimbali.
Mohamed Bwanali alisema, kuna watumishi wamekaa na kufanya kazi katika kijiji hicho kwa muda mrefu,kwa hiyo wanafanya kazi kwa mazoea jambo linalosababisha hata miradi inayopelekwa na Serikali kutosimamiwa vizuri.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.