Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Ruvuma, Mheshimiwa Jakline Msongozi, leo Mei 6, 2025, amelipamba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hotuba yake yenye msisitizo mkubwa kuhusu hali ya miundombinu ya barabara mkoani Ruvuma, akichangia bajeti ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka 2025/2026.
Akiwa amejaa shukrani na pongezi, Msongozi ameanza kwa kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ya kuboresha miundombinu nchini, huku akimpongeza pia Waziri wa Ujenzi na Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Saleh Juma, kwa usimamizi mzuri wa miradi ya barabara katika mkoa huo.
Akiweka bayana kilio chake kikuu, Mbunge huyo ameitaka serikali kutoa majibu ya kina kuhusu hatma ya barabara ya mchepuko ya Songea Mjini yenye urefu wa kilometa 16, akieleza kuwa amekuwa akiuliza swali hilo mara kadhaa bungeni bila kupata majibu yanayoridhisha. “Naibu Waziri alisema mkandarasi yuko kazini, lakini wananchi hawajashuhudia mwanzo wa ujenzi,” alisema.
Msongozi pia amegusia barabara ya kutoka Songea hadi Makambako yenye urefu wa kilometa 395, akieleza kuwa barabara hiyo imejaa mabonde na viraka, hali inayosababisha wasafiri kutumia hadi saa saba kwa safari inayopaswa kuchukua saa nne pekee. “Barabara hii ina maroli mengi ya makaa ya mawe, ni lazima ijengwe kwa haraka,” alisisitiza.
Kwa upande mwingine, Mbunge huyo ameonesha hofu juu ya kutotekelezwa kwa ujenzi wa barabara ya kimkakati ya Likuyufusi–Mkenda wilayani Songea, inayounganisha Tanzania na Msumbiji. Alisema licha ya kutengewa Shilingi bilioni 60 kwa ajili ya kilometa 60, hadi sasa hakuna hata kilometa moja iliyojengwa.
Katika wilaya ya Namtumbo, Msongozi alielezea kusikitishwa kwake na kutoanza kwa ujenzi wa barabara ya Lumecha–Londo–Mpepo yenye urefu wa kilometa 300, akiitaka serikali itangaze tarehe rasmi ya kuanza ujenzi huo ili kutoa matumaini kwa wananchi waliokuwa wakisubiri kwa muda mrefu.
Aidha, ameitaja barabara ya kimkakati ya Mtwara–Pachani hadi Tunduru yenye urefu wa kilometa 305 kuwa ni muhimu kwa maendeleo ya biashara na usafirishaji katika mikoa ya kusini, akisema hakuna taarifa za wazi kuhusu kuanza kwa ujenzi wake.
Katika hatua nyingine, Msongozi alipongeza hatua ya serikali kuanza kujenga daraja la Mkili wilayani Nyasa, akisema hatua hiyo imeleta matumaini makubwa kwa wananchi wa Nyasa, lakini akasisitiza kuwa barabara ya Mbambabay–Lituhi inayopita kandokando ya Ziwa Nyasa bado inahitaji ujenzi wa haraka kutokana na umuhimu wake wa kiulinzi na kiutalii.
Mbunge huyo aliitaka serikali kuweka kipaumbele katika ujenzi wa barabara ya Kigonsera–Mbaha kilometa 56, barabara ya Kitai–Ruanda kilometa 40 wilayani Mbinga, na kuikamilisha hadi Ndumbi wilayani Nyasa, akisema barabara hizo ni kiungo muhimu kwa uchumi na usalama wa wakazi wa Ruvuma na mikoa jirani.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.