MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Ruvuma (CCM) Mheshimiwa Mariam Nyoka,amemtembelea Mwalimu wa shule ya msingi Wenje kata ya Nalasi Magharibi Halmashauri ya wilaya ya Tunduru Judith Sichalwe aliyejifungua watoto wanne mapacha mwezi Mei mwaka jana.
Mwalimu Judith Schalwe,anahitaji msaada wa hali na mali ili aweze kuwalea na kuwahudumia watoto wake watatu waliobaki baada ya mmoja kufariki dunia mwezi Septemba mwaka uliopita.
Akizungumza baada ya kukabidhi msaada wa vitu mbalimbali kwa Mwalimu Judith,Nyoka amewataka wadau na wananchi wenye uwezo kujitokeza kumsaidia mwalimu huyo ili aweze kuwalea watoto wake watatu.
Amesema licha ya Judith kuwa mtumishi wa umma,lakini bado anakabiliwa na changamoto kubwa ya kimaisha,hivyo jamii inapaswa kumshika mkono kwa kumpa kile walichonacho kwa sababu kazi ya kulea watoto watatu mapacha ni ngumu.
Nyoka, ametoa msaada wa vitu mbalimbali ikiwamo Pampasi,sabuni za kufulia na kuogea,unga wa mahindi,mafuta ya kupata,sukari,nguo na fedha taslimu ambazo zitatumika kumsaidia na kuwatunza watoto hao na amehaidi kumpa Pikipiki Mwalimu huyo ili iweze kuwaingizia kipato.
Katika hatua nyingine Nyoka,ametoa msaada wa baiskeli ya magurudumu matatu kwa mkazi wa mtaa wa Mlingoti Magharibi Sophia Ali mwenye ulemavu wa miguu.
Sophia Ali licha ya kuwa mlemavu anayehitaji msaada wa wasamaria wema,ni mama wa watoto saba kati ya hao watoto wanne ni walemavu ambao wanahitaji msaada wa hali na mali ili iweze kuwasaidia.
Kwa upande wake Mwalimu Judith,amemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kumsaidia kwa kumpa ajira ya Ualimu Baba watoto wake Hamis Shaibu ambaye ana Diploma ya Ualimu, lakini hadi sasa hajapata kazi licha ya kutuma maombi mara kwa mara serikalini.
Amesema,anakabiliwa na hali ngumu ya maisha kwani hata mshahara anaopata hautoshelezi kwa kuwa sehemu kubwa ya fedha hizo zinatumika kwa ajili ya matunzo ya watoto wake.
Mwalimu Judith,ameshukuru Mbunge huyo kwenda kumuona na kumpa msaada wa vitu mbalimbali kwa ajili ya watoto wake na kuwaomba wadau wengine kumsaidia
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.