MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Ruvuma Mheshimiwa Jacqueline Msongozi ameishauri serikali kupitia Wizara ya Nishati kuangalia uwezekano wa kuweka ruzuku kwenye mitungi ya gesi ya kupikia ili kupunguza bei ya mitungi hiyo kwa wananchi.
Akizungumza Bungeni jijini Dodoma Mbunge huyo ameshauri serikali kuongea na wadau mbalimbali ili kuondoa gharama kubwa ya ununuzi wa mitungi ya gesi ya kupikia wakati mchakato wa kupunguza gesi hiyo unaendelea serikalini.
Amesema gesi ya asilia inapunguza gharama kubwa kwa matumizi ya kupikia ukilinganisha na matumizi ya kuni na mkaa ambavyo vinagharama kubwa pia vinachafua mazingira.
Ameshauri serikali kuangalia namna inavyoweza kuweka mfumo wa gesi asilia kwenye Taasisi zote za serikali kikiwemo Chuo cha Ualimu Matogoro Songea na katika shule za sekondari mkoani Ruvuma na nchi nzima kwa ujumla.
Akizungumza bungeni Dodoma Naibu Waziri wa Nishati Mheshimiwa Judith Kapinga amesema agenda ya nishati safi ya kupikia ni ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan hivyo Wizara ya Nishati imelibeba suala hilo kwa uzito wa kipekee.
Kuhusu Ruzuku kwenye nishati safi ya kupikia,amesema kuna program inayowawezesha mawakala kuwezeshwa kifedha ili kupunguza bei ya mitungi ya gesi kwa wanaonunua gesi kwa mara ya kwanza.
“Serikali itaendelea kubuni miradi ya kupunguza bei ya mitungi ya gesi na kutafuta fedha ili kuhakikisha wananchi wanapata mitungi ya gesi kwa gharama rahisi zaidi’’,alisisitiza Naibu Waziri wa Nishati.
Kuhusu kuwekeza mifumo ya gesi asilia kwenye Taasisi ,Mheshimiwa Kapinga amesema kupitia Wakala wa Nishati vijijini REA umeanzishwa mradi kwa ajili ya kuweka nishati safi ya kupikia ya gesi kwenye magereza,kambi za jeshi Pamoja na shule za msingi na sekondari.
Hata hivyo amesema Wizara itaendelea kutafuta fedha ili kuhakikisha mifumo ya nishati safi ya kupikia inazifikia Taasisi nyingi zaidi zikiwemo Taasisi za elimu mkoani Ruvuma.
Sera ya Taifa ya mwaka 2015 inaielekeza serikali kuchukua hatua Madhubuti ili kufanikisha matumizi ya nishati safi,
Hivi sasa serikali inakamilisha kuandaa mkakati wa Taifa wa matumizi safi ya nishati ya kupikia kwa lengo la kuhakikisha asilimia 80 ya watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2033.
Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini GCU Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvum
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.