MFUMO wa stakabadhi ghalani umewaingizia wakulima wa Wilaya za Songea na Namtumbo mkoani Ruvuma mabilioni ya fedha tangu ulipoanza kutumika mwaka 2019.
Akizungumza wakati anatoa taarifa ya uendeshaji wa Chama Kikuu cha Ushirika SONAMCU Ltd kwa Mkuu wa Mkoa wa Mkoa wa Ruvuma,Meneja Mkuu wa Chama hicho Juma Mwanga amesema wakulima wamepata mafanikio makubwa katika mazao ya ufuta,soya na mbaazi yaliouzwa kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani.
Mwanga amesema katika kipindi cha mwaka 2019 hadi 2021,kupitia zao la ufuta,wakulima waliuza kilo 19,163,454 na kufanikiwa kupata zaidi ya shilingi bilioni 45,huku Halmashauri zikipata mapato ya zaidi ya bilioni 1.9,SONAMCU ilipata zaidi ya milioni 574 na vyama vya msingi zaidi ya shilingi bilioni1.341.
Amesema katika kipindi hicho cha miaka mitatu katika zao la soya ziliuzwa jumla ya kilo 5,550,290 na wakulima kuingiza zaidi ya shilingi bilioni 4.925,mapato ya Halmashauri zaidi ya shilingi milioni 156,SONAMCU zaidi ya milioni 84 na mapato ya vyama vya msingi ni zaidi ya milioni 194.
Kulingana na Meneja Mkuu huyo wa SONAMCU,katika kipindi cha mwaka 2019 hadi 2021 katika zao la mbaazi kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani ziliuzwa kilo 4,920,996 ambazo ziliwaingizia wakulima zaidi ya shilingi bilioni nne,Halmashauri ilipata zaidi ya shilingi milioni 143,SONAMCU ilipata zaidi ya milioni 59 na vyama vya msingi vilipata zaidi ya shilingi milioni 129.
“Mfumo wa stakabadhi ghalani una faida nyingi zikiwemo wakulima kukutanishwa na wanunuzi hivyo kuwafanya wawe na maamuzi ya kuuza mazao yao kwa umoja wao na kuwepo kwa matumizi ya vipimo halali vya wakulima kwa sababu wanunuzi hutumia mizani iliyohakikiwa na wakala wa vipimo’’,alisisitiza Mwanga.
Amezitaja faida nyingine za mfumo huo kuwa ni upatikanaji wa tozo za serikali kwa njia rahisi,kuongezeka kwa bei ya mazao ya ufuta,soya na mbaazi ambao umetokana na kuongezeka kwa wanunuzi ambao wanashindanishwa kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani na kutoa bei kubwa kwa wakulima.
Faida nyingine za mfumo huo ni kufufuka kwa vyama vya ushirika toka 24 vilivyokuwa vinauza tumbaku tu hadi kufikia 63 ambavyo vinauza mazao ya ufuta,soya na mbaazi.
Chama kikuu cha SONAMCU ambacho kiliandikishwa mwaka 2013 hivi sasa kina wanachama 46 wa vyama vya msingi.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge ametoa rai kwa vyama vya ushirika kuendelea kutoa elimu ya faida kwa mfumo huo kwa wanachama wao ili wakulima wengi wautumie na kupata bei yenye tija.
Ametoa rai kuangalia wakulima wengi zaidi kujiunga na mfumo huo ili kupata tija katika mazao yao hivyo ameagiza vyama vya kushirika kuongeza uaminifu kwa watendaji na kuzingatia maslahi ya wanachama ambapo ametaka kuachana na maslahi binafsi ambayo yanarudisha nyuma ushirika.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Septemba Mosi,2021
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.