BEI ya kuuza mbaazi za wakulima katika wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani imezidi kupanda zaidi kutoka wastani wa Sh.1,294 hadi kufikia Sh.1,341 kwa kilo moja.
Afisa Ushirika wa wilaya ya Tunduru George Bisani amesema,katika minada yote miwili jumla ya kilo 1,505,849 kati ya hizo kilo 360,551 zimeuzwa katika mnada wa kwanza kwa bei ya Sh.1,294 kwa kilo moja.
Amesema, katika mnada wa pili uliofanyika katika kijiji cha Semeni jumla ya kilo 1,145,498 zimeuzwa kwa bei ya Sh.1,391 na kufanya jumla ya fedha zote zilizoingia kwenye mzunguko kutokana na minada miwili ya mbaazi wilayani Tunduru kufikia Sh. Bilioni 1,536,167,320.00.
Kwa upande wake Meneja Mkuu wa Chama Kikuu cha Ushirika wilaya ya Tunduru(Tamcu Ltd)Imani Kalembo amesema, huo ni mnada wa pili wa zao la mbaazi kufanyika katika wilaya hiyo katika msimu wa kilimo wa mwaka 2020/2021.
Kalembo amesema, katika mnada huo makampuni matano yamejitokeza kununua mbaazi na kampuni ya Lenic Tanzania Ltd imeshinda kutokana na kutangaza bei ya Sh.1,341 kwa kilo moja ikiyazidi makampuni mengine.Amesema, katika mnada huo jumla ya tani 1,042 sawa na kilo 1,145,498 zimeuzwa ambapo bei ya kilo moja ya mbaazi ni Sh. 1,341.
Amesema, Chama Kikuu cha Ushirika kina furaha kuona bei ya mbaazi inaongezeka katika kila mnada kutoka Sh.1,294 katika mnada wa kwanza uliofanyika katika kijiji cha Mtonya hadi kufikia Sh 1,341 mnada wa pili uliofanyika kijiji cha Semeni.
Amewataka wakulima kutokubali kushawishika na wanunuzi wa kati wanaonunua mbaazi kwa bei ndogo ya Sh. 800 kwa kilo ambayo haina faida, badala yake kuendelea kuuza mbaazi zao mfumo wa stakabadhi ghalani kupitia vyama vya msingi vya ushirika.
Ametoa wito kwa makampuni mbalimbali,kwenda katika wilaya hiyo kununua mbaazi ambazo zinapatikana kwa wingi na kuhakikisha wananunua kwa bei nzuri ili kuhamasisha wakulima waweze kuzalisha kwa wingi.
Baadhi ya wakulima wa mbaazi katika kijiji hicho wameishukuru Serikali kwa kuliingiza zao hilo katika mfumo wa stakabadhi ghalani kwa kuwa umewasaidia kupata soko la uhakika na bei nzuri kutoka Sh. 250 hadi 300 kwa kilo moja.
Wamesema, kuanzishwa kwa mfumo wa stakabadhi ghalani kwa zao la mbaazi na mazao mengine ya kimkakati ikiwemo zao maarufu la korosho kumewasaidia kuwa na uhakika wa bei nzuri na kuepuka kulanguliwa na wanunuzi wa mitaani wasiokuwa na huruma kwao.
Hadija Omari(43)amesema, kama serikali itaendelea na kusimamia mpango wa kuuza mbaazi kwa mfumo wa stakabadhi ghalani basi wakulima wengi watahamasika kuongeza uzalishaji na hivyo kuondokana na umaskini katika familia zao.
Ameitaka Serikali kuhakikisha inawabana na kuwachukulia hatua kali baadhi ya wanunuzi wachache wanaopita mashambani na vijijini kuwalaghai wakulima, ili wauze mbaazi kwa bei ndogo isiyolingana na gharama halisi za uzalishaji.
Omari Misoya amesema, licha ya malipo kuchelewa mara wanapouza,lakini mfumo wa stakabadhi ghalani umesaidia kupata bei nzuri ya mbaazi wanazolima ikilinganisha na bei za walanguzi wa mitaani.
Amesema,mfumo huo umeleta heshima kubwa kwa mkulima na pia usalama wa fedha wanazolipwa kwani zinapitia moja kwa moja benki badala ya kupewa mkononi jambo ambalo ni hatari kwa maisha yao.Hata hivyo, ameiomba Serikali kuyabana makampuni yanayonunua mbaazi kulipa fedha kwa wakulima haraka ili waweze kutatua changamoto zinazowakabili kwenye familia zao mahitaji ya shule kwa Watoto wao.
Imeandikwa na Muhidin Amri Tunduru
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.