WAKULIMA wa mazao ya ufuta,mbaazi na korosho wanaohudumiwa na Chama Kikuu cha Ushirika wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma(TAMCU),katika msimu wa kilimo wa mwaka 2022/2023 wamelipwa zaidi ya Sh.bilioni 33 kupitia vyama vya msingi vya ushirika(Amcos).
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa TAMCU Mussa Manjaule wakati akitoa taarifa ya chama hicho kwenye mkutano mkuu wa Tamcu uliofanyika katika ukumbi wa Sky Way mjini Tunduru.
Manjaule alisema,Chama kikuu cha Ushirika(Tamcu Ltd)kinachosimamia mauzo ya zao la korosho katika mikoa ya Njombe,Ruvuma na Mbeya katika msimu wa kilimo 2022/2023 kilifanikiwa kukusanya jumla ya kilo 20,802,513 ya mazao matatu ya Ufuta,mbaazi na korosho ambapo kati ya hizo korosho zilikuwa kilo 15,218,006 zenye thamani ya Sh.bilioni 26,917,916,197.03 na wakulima walilipwa Sh.bilioni 23,312,161,64.
Alisema,kwa upande wa zao la ufuta walikusanya kilo 2,548,815 zenye thamani ya Sh.bilioni 7,710,907,700.00 ambazo ziliwaingizia wakulima Sh.bilioni 7,498,081,647.5 na mbaazi zilipatikana kilo 3,035,692 zenye thamani ya Sh.bilioni 2,633,233,689.53 na wakulima walilipwa Sh.bilioni 2,475,377,705.5.
Aidha alisema,katika msimu wa kilimo 2022/2023 licha ya kuwa na hali mbaya ya hewa iliyoambatana na mvua zisizoeleweka ambayo kwa kiasi kikubwa ilichangia kupunguza ubora wa mazao hasa korosho wakati wa uvunaji,lakini wamefanikiwa kudhibiti ubora wa mazao.
Kwa mujibu wa Manjaule,hali hiyo imetokana na usimamizi na operesheni za mara kwa mara zilizofanywa na kamati ya ulinzi na usalama ikiongozwa na Mkuu wa wilaya Julius Mtatiro kwa kushirikiana na wajumbe wa bodi ya Tamcu Ltd na vyama vya Ushirika vya msingi.
Alisema kuwa,ushuhuda wa ubora wa mazao hayo uliwavutia hata wanunuzi ambao walikiri kuwa ni safi ambapo kwa upande wa korosho kati ya kilo 15,218,006 zilizouzwa mnadani kilo 14,845,624 zilikuwa daraja la kwanza na kilo 372,382 daraja la pili.
Kwa upande wake meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika wilayani humo(Tamcu Ltd)Iman Kalembo alisema,katika msimu 2022/2023 Tamcu imeendesha jumla ya minada 11 ya mauzo ya korosho ghafi na kuuza kilo 15,281,006 zenye thamani ya Sh.bilioni 26,291,272,829.
Alifafanua kuwa,kati ya kilo hizo mkoa wa Ruvuma ulizalisha kilo 15,156,209 sawa na asilimia 99.5,mkoa wa Njombe ulizalisha kilo 35,947 sawa na asilimia 0.24 na kilo25,850 sawa na asilimia 0.17 zilitoka mkoa wa Mbeya.
Alisema,uzalishaji wa korosho umeshuka kutoka kilo 25,284,493 kwa msimu 2021/2022 hadi kilo 15,218,006 kwa msimu 2022/2023 ambapo ni sawa na anguko la asilimia 39.81.
Kalembo alisema,changamoto ya kushuka kwa uzalishaji na ubora wa korosho,ilichangia hata kushuka kwa bei katika soko la Dunia ambapo korosho daraja la kwanza iliuzwa kwa bei ya juu Sh. 1,905 na ya chini Sh.1,600 na kufanya wastani wa bei kwa korosho za daraja la kwanza Sh. 1,742 na daraja la pili bei ya juu Sh.1,370 na bei ya chini Sh.1,340.
Aliongeza kuwa, wastani wa bei ya korosho kwa msimu 2022/2023 ni Sh.1,357 ikilinganishwa na msimu 2021/2022 ambapo korosho zote ziliuzwa daraja la kwanza na bei ya juu ilikuwa Sh.2,157 na bei ya chini Sh.1,700.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro,amewapongeza wakulima kwa kuendelea na uzalishaji wa zao hilo na viongozi wa vyama vya msingi na Chama Kikuu cha Ushirika(Tamcu Ltd)kwa usimamizi mzuri na kumaliza madeni ya fedha za wanachama wao.
Alisema,hali hiyo imetokana na viongozi waliopo kufuata kanuni,sheria na taratibu za Ushirika ambazo zimesaidia kuimarisha sana Amcos na wakulima kulipwa stahiki zao,tofauti na miaka ya nyuma ambapo kulikuwa na ubabaishaji mkubwa kila inapofika wakati wa msimu wa mauzo ya korosho.
Amewataka viongozi wanaosimamia vyama vya ushirika,kuwa waadilifu,waaminifu,kutenda haki na kutekeleza majukumu yao kwa wakati, badala ya kuvitumia vyama hivyo kama taasisi ya familia au sehemu ya kutafuta nafasi za uongozi.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.