Na Albano Midelo
Katika miaka minne iliyopita, sekta ya afya nchini Tanzania, hasa katika mkoa wa Ruvuma, imepiga hatua kubwa kwa juhudi za serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dr.Louis Chomboko anasema Kupitia uwekezaji wa miundombinu, rasilimali watu, na huduma za afya za msingi, maendeleo yamekuwa dhahiri huku wananchi wakishuhudia maboresho makubwa katika upatikanaji wa huduma bora za afya.
Ongezeko la Vituo vya Afya na Rasilimali Watu
Mkoa wa Ruvuma una jumla ya vituo 473 vya huduma za afya, ikiwa ni pamoja na hospitali 18, vituo vya afya 50, na zahanati 341.
Hata hivyo Serikali inamiliki sehemu kubwa ya vituo hivi, ikiwa na hospitali tisa, vituo vya afya 39, na zahanati 277. Pamoja na ongezeko hili, upatikanaji wa watumishi wa afya uko katika asilimia 47.2 huku mahitaji yakiwa watumishi 7,043 dhidi ya waliopo 3,323.
Maboresho ya Huduma za Afya Kupitia Teknolojia
Katika kuhakikisha huduma za afya zinaboreshwa, mfumo wa kielektroniki wa serikali (GoTHOMIS) umesimikwa katika vituo 192 kati ya 325, sawa na asilimia 64.74, huku lengo likiwa ni kufikia vituo vyote.
Upatikanaji wa Dawa na Vifaa Tiba
Upatikanaji wa dawa na vifaa tiba umeongezeka kutoka asilimia 50 mwaka 2021 hadi asilimia 84 mwaka 2024. Hii ni kutokana na usimamizi thabiti wa serikali, pamoja na ongezeko la ruzuku kwa vituo vya afya.
Kiasi cha shilingi bilioni 7.95 kilitolewa kwa ajili ya dawa na vifaa tiba, huku asilimia 90.1 ya bidhaa zilizohitajika zikifikishwa kwenye vituo vya afya.
Mafanikio Katika Huduma za Chanjo
Katika kipindi cha miaka minne, huduma za chanjo zimeimarika, huku baadhi ya chanjo zikifikia viwango vya juu zaidi ya asilimia 100 ya malengo yaliyowekwa. Mfano, chanjo ya kifua kikuu (BCG) imefikia asilimia 166, polio asilimia 135, na HPV asilimia 126.
Huduma za Uzazi na Mtoto
Mkoa wa Ruvuma una vituo 348 vinavyotoa huduma za afya ya uzazi na mtoto, ambapo vituo 325 vinatoa huduma ya chanjo na vituo 313 vinatoa huduma ya uzazi na kujifungua.
Huduma za Saratani ya Mlango wa Kizazi
Jumla ya wanawake 22,718 walichunguzwa saratani ya mlango wa kizazi, ambapo 301 (asilimia 1.3) waligundulika kuwa na VIA positive na asilimia 87 walitibiwa. Wanawake 79 walihisiwa kuwa na saratani na kupatiwa rufaa kwa uchunguzi zaidi.
Huduma za Ustawi wa Jamii na Mfuko wa Afya (iCHF)
Mpango wa usajili wa watoto chini ya miaka mitano umefanikiwa kwa asilimia 119.9, huku watoto 283,094 wakiwa wameandikishwa. Aidha, kaya 31,767 zimejiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii ulioboreshwa (iCHF), zikichangia shilingi milioni 953 .
Uwekezaji katika Huduma za Maabara na Uchunguzi wa Magonjwa
Mkoa umepokea mashine za kisasa za uchunguzi wa magonjwa, ikiwa ni pamoja na mashine 27 za hematolojia, 26 za biochemistry, mashine tisa za Genexpert kwa uchunguzi wa kifua kikuu na mashine nane za X-ray za kidijitali ambazo zimepelekwa kwenye hospitali mbalimbali.
Maendeleo ya Miundombinu ya Afya
Serikali imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 4.76 katika miradi 29 ya afya, ambapo miradi 2 imekamilika kwa asilimia 100 na mingine 27 ipo katika hatua mbalimbali za umaliziaji. Kwa mwaka 2024/2025, Tsh 3.42 bilioni zimetengwa kwa miradi mipya.
Mafanikio haya yanaonesha dhamira ya serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha sekta ya afya, kwa maendeleo endelevu ya sekta ya afya nchini Tanzania.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.