JAJI Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Songea Mheshimiwa James Karayemaha amesema mifumo ya utoaji na upatinaji haki nchini ni muhimu kuboreshwa na kuimarishwa ili iweze kuleta usawa na ustawi katika jamii.
Jaji Karayemaha amesema hayo wakati anazungumza kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya sheria nchini ambazo kimkoa zimefanyika kwenye viwanja vya Mahakama Kuu Kanda ya Songea.
Amebainisha kuwa utoaji na upatikanaji wa haki utawezekana ikiwa kutakuwa na mifumo imara na jumuishi baina ya Taasisi hususan kwenye eneo la vitendea kazi vya kisasa vya TEHAMA na uwepo wa miundombinu wezeshi baina ya Taasisi ya haki jinai.
“Mahakama imekuwa ikifanya maboresho kwenye huduma zake ili kutoa huduma bora inayomlenga mwananchi kupitia Mpango Mkakati wa miaka mitano ambao umesimikwa katika nguzo tatu zinazoongoza katika utekelezaji na Programu za kimaboresho’’,alisisitiza Jaji Mfawidhi.
Amezitaja nguzo hizo kuwa ni mahakama kutekeleza utawala bora,uwajibikaji na usimamizi wa rasilimali,upatikanaji na utoaji wa haki kwa wakati na kuthamini imani kutoka kwa wananchi,watumiaji wa huduma za mahakama na jamii kwa ujumla.
Akizungumzia umuhimu wa mfumo jumuishi Jaji Mfawidhi huyo Mahakama Kuu Kanda ya Songea,amesisitiza kuwa kuanzishwa kwa Mfumo Jumuishi wa Taasisi za Haki Jinai utasaidia upatikanaji wa taarifa kwa wakati muafaka,kuondoa urasimu na utendaji kazi katika hatua mbalimbali zilizopo kwenye Taasisi za Haki Jinai hivyo haki kutolewa kwa wakati.
Hata hivyo amesema TEHAMA ina nafasi kubwa katika kuboresha haki na kufanikisha upatikanaji wa haki kwa wakati ambapo amesema Mahakama inaendelea kuboresha huduma zake kupitia mifumo ya TEHAMA.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas akizungumza kwenye kilele cha maadhimisho hayo ameipongeza Idara ya Mahakama Kuu Kanda ya Songea kwa kupiga hatua kubwa katika utoaji haki hasa baada ya kuboresha miundombonu ya mahakama ikiwa ni Pamoja na matumizi ya TEHAMA.
RC Thomas ameipongeza Mahakama Kuu Kanda ya Songea kwa kutatua changamoto ya mlundikano wa mashauri ambapo hivi sasa mashauri yenye muda mrefu yamebakia machache.
Ameipongeza Mahakama hiyo kwa kupeleka vifaa vya TEHAMA katika magereza ya Tunduru na Mbinga ambavyo vinakwenda kutumika kwa ajili mfumo wa jumuishi wa haki jinai kwa ajili ya kusikiliza mashauri kwa njia ya mtandao.
Amesisitiza kuwa juhudi zinazofanywa na vyombo vyote vya haki jinai zina mchango mkubwa kwa jamii ambapo ameshauri kushirikiana ili kuunganisha mifumo ya utendaji kazi hatimaye kufikia mafanikio makubwa katika utoaji haki.
Kaulimbiu ya mwaka huu kwenye maadhimisho ya siku ya sheria nchini inasema umuhimu wa dhana ya haki kwa ustawi wa Taifa;nafasi ya mahakama na wadau katika kuboresha mfumo jumuishi na haki jinai.Baadhi ya Mahakimu kutoka Kanda ya Songea wakiwa kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya sheria nchini
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.