SERIKALI imetumia kiasi cha Sh.milioni 110 kukamilisha ujenzi wa Bweni la wanafunzi wa kike katika shule ya sekondari Chabruma kata ya Lilambo katika manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa bweni hilo kwa Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanal Laban Thomas,Mkuu wa shule hiyo Sikudhan Komba alisema ujenzi wa bweni hilo umetekelezwa kwa awamu tatu.
Komba alisema,katika awamu ya kwanza kwa mwaka wa fedha 2020/2021 walipokea Sh.milioni 80
ikiwa ni fedha za mradi EP4R.Alisema,katika awamu ya pili mwaka 2021/2022 walipokea Sh.milioni 8 kutoka mfuko wa Jimbo na awamu ya tatu 2022/2023 wamepokea Sh.milioni 22 fedha kutoka serikali kuu.
Alisema,kukamilika kwa mradi huo kumewasaidia watoto wa kike 74 kuishi bwenini na hivyo kupunguza adha ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kutoka maeneo wanayoishi.
Aidha alisema,wanafunzi wanapata muda wa ziada wa kujisomea,kuepukana vishawishi mbalimbali,kuongeza ufaulu na utawasaidia wanafunzi wa kike kuweza kutimiza ndoto zao.
Akizungumza baada ya kuzindua bweni hilo Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanal Laban Thomas,amewataka wanafunzi kusoma kwa bidii ili waweze kutimiza ndoto zao na kuepuka kupokea zawadi kwa watu wenye nia ovu hasa kwa watoto wa kike.
Alisema,serikali ya awamu ya sita imejitahidi sana kujenga na kuboresha miundombinu ya elimu inayomsaidia mwanafunzi kusoma katika mazingira mazuri na walimu kuwa na sehemu nzuri ya kufundishia.
Kanal Laban,amewaasa wanafunzi kuzingatia masomo na kuzingatia maadili ya kitanzania na kuepuka kujiingiza kufanya vitendo vinavyokwenda kinyume na maadili ambavyo kwa sehemu kubwa vina wadhalilisha hasa vijana wa kiume kutokana na tamaa ya kupata mali.
Amewataka wanafunzi kutunza bweni hilo na miundombinu mingine ya shule,ili iweze kudumu kwa muda mrefu na iwasaidie katika kutimiza ndoto zao badala ya kuwa sehemu ya waharibifu wa miundombinu hiyo inayojengwa kwa fedha nyingi za serikali.
Katika hatua nyingine Mkuu wa mkoa,amewakumbusha Watanzania kuhusu umuhimu wa kudumumisha muungano na amani ya nchi yetu kwa kutokubali kushawishiwa kwa namna yoyote kujaribu kuvunja muungano wetu ambao ni mawazo mazuri ya waasisi wa Taifa letu Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Aman Karume.
“wanangu mjitahidi kusoma kwa bidii kwani elimu ndiyo itawakomboa katika maisha yenu,elimu ndiyo itatufanya tuendelea kudumisha na kusimamia muungano wetu kwa kujua faida na manufaa yake,tusiposoma itakuwa rahisi kudanywa kuhusu muungano wetu”alisema Kanal Laban.
Alisema,muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni wa aina yake Duniani na haupatikani sehemu yoyote na unatoa fursa kwa kila Mtanzania kuwa na haki ya kuwekeza kitu chochote ndani ya Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.